Jul 09, 2019 08:20 UTC
  • Wayemen karibu nusu milioni wanakabiliwa na kipindupindu

Wimbi jipya la maradhi ya kipindupindu linashuhudiwa nchini Yemen ambapo kesi zaidi ya 460,000 za maradhi hayo zimeripotiwa kuanzia Januari mwaka huu hadi sasa.

Hayo yamesemwa na Farhan Haq, Naibu Msemaji wa Umoja wa Mataifa ambaye ameongeza kuwa, katika kipindi hicho cha kuanzia Januari hadi sasa, Wayemen zaidi ya 700 wameaga dunia kutokana na ugonjwa huo hatari.

Takwimu hizo mpya zinaashiria ongezeko la kutisha la maambukizi ya ugonjwa huo, kwani katika kipindi cha Januari hadi Juni mwaka jana ni watu 75 tu walipoteza maisha kutokana na ugonjwa huo nchini Yemen, na kesi 380,000 kuripotiwa. 

Viongozi wa Yemen wamenukuliwa na duru za habari wakithibitisha madai ya kuhusika kwa namna moja au nyingine muungano vamizi wa kijeshi unaoongozwa na Saudi Arabia katika kuenea maradhi ya kipindupindu katika nchi hiyo maskini ya Kiarabu.

Wayemen wakitibiwa kipindupindu katika hospitali isiyo na vitanda na suhula nyinginezo

Itakumbukwa kuwa Saudia kwa kushirikiana na Marekani, Israel, Imarati na baadhi ya nchi za Magharibi na Kiarabu ilianzisha mashambulizi makali ya kila upande dhidi ya Yemen hapo mwezi Machi 2015 sambamba na kuizingira nchi hiyo masikini ya Kiarabu kwa pande za nchi kavu, baharini na angani.

Vita vya Saudia na washirika wake nchini Yemen hadi sasa vimepelekea mauaji ya makumi ya maelfu ya watu huku malaki ya wengine wakijeruhiwa mbali na mamilioni ya wengine kulazimika kuwa wakimbizi.

Tags