Baraza la Maulama Saudia lapinga ufisadi wa kimaadili nchini humo
(last modified Tue, 09 Jul 2019 12:52:44 GMT )
Jul 09, 2019 12:52 UTC
  • Baraza la Maulama Saudia lapinga ufisadi wa kimaadili nchini humo

Wajumbe watatu wa Baraza la Maulama nchini Saudi Arabia wamekataa kushiriki katika vikao vya baraza hilo wakilalamikia ufuska na ufisadi wa kimadili nchini humo.

Hayo yameripotiwa na mhadhiri wa chuo kikuu na mwanaharakati wa kisiasa wa Saudi Arabia, Said bin Nasir al Ghamidi ambaye ingawa hakutaja majina ya wanazuoni hao, ameandika katika ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Twitter kwamba: Wasomi hao wameamua kudhihirisha malalamiko yao kwa njia hiyo kwa sababu hawaruhusiwi kuzungumzia ufuska na ufisadi wa kimaadili ulioenea nchini Saudi Arabia.

Wakati huo huo wanaharakati wa mitandao ya kijamii nchini humo wanatumia nara ya "Taasisi ya Burudani na Starehe ya Saudi Arabia inadhalilisha Misikiti" kupinga na kuonesha hasira zao dhidi ya kazi zinazofanywa na taasisi hiyo.

Nara hiyo imeanzishwa baada ya Taasisi ya Burudani na Starehe ya Saudi Arabia kumwalika mwanamuziki wa Kimarekani, Nicky Minaj kushiriki katika tamasha la muziki la mjini Jeddah.

Wanaharakati wa mitandao ya kijamii na wananchi wa Saudi Arabia wamelalamikia vikali tamasha hilo na kusema kuwa, litamkaribisha mwanamuziki wa RAP wa Kimarekani anayecheza uchi jukwaani na kupinga vikali siasa za mabadiliko za mrithi wa kiti cha ufalme wa Saudia, Mohamed bin Salman. 

Nicky Minaj

Tamasha la muziki la Jeddah linatarajiwa kufanyika tarehe 17 Julai mwaka huu chini ya usimamizi wa Taasisi ya Burudani na Starehe ya Saudi Arabia ambapo mwanamuziki Nicky Minaj anatarajiwa kutumbuiza.

Taasisi ya Burudani na Starehe ya Saudi Arabia ni sehemu ya miradi iliyoanzishwa na Bin Salman katika kile kinachotajwa kuwa ni mabadiliko ya kijamii, kiuchumi na kisiasa nchini Saudi Arabia.

 Mabadiliko yake ya kijamii yanaiga vigezo vya madola ya Magharibi visivyo vya Kiislamu na visivyo vya kimaadili, jambo ambalo linalalamikiwa vikali na Waislamu kote ulimwenguni.

Tags