Aoun: Kuiwekea vikwazo Hizbullah ni kuivunjia heshima Lebanon
Rais wa Lebanon amesema kuwa vikwazo vya Marekani dhidi ya wawakilishi wa harakati ya Hizbullah ya nchi hiyo ni sawa na kuivunjia heshima Lebanon.
Rais Michel Aoun ameitaka serikali ya Marekani kufutilia mbali vikwazo vyake dhidi ya wawakilishi wa Hizbullah katika Bunge la Lebanon. Rais wa Lebanon ameongeza kuwa, vikwazo vya Marekani dhidi ya wabunge wa Hizbullah vinakinzana na misimamo ya huko nyuma ya Marekani ambayo inathibitisha kuwa Lebanon na benki za nchi hiyo zinaheshimu sheria za kupambana na utakatishaji wa pesa chafu.
Nabih Berri Spika wa Bunge la Lebanon pia amekosoa hatua hiyo ya Washington dhidi ya wabunge la Hizbullah na kueleza kuwa nvikwazo vya Marekani dhidi ya wawakilishi hao wa Hizbullah bungeni ni ukiukaji wa mamlaka ya ya kujitawala ya Lebanon. Wizara ya Fedha ya Marekani hivi karibuni iliongeza majina ya wabunge kadhaa wa harakati ya Hizbullah katika orodha mpya ya vikwazo vyake na kuitaka serikali ya Lebanon kukata uhusiano wake na wabunge hao.
Marekani imechukua hatua hiyo dhidi ya Hizbullah katika hali ambayo kundi hilo linaungwa mkono pakubwa na wananchi wa Lebanon.