Mousa Abu Marzook: Jeuri ya Marekani mkabala na Iran haikubaliki
Mousa Mohammed Abu Marzook, kiongozi mwandamizi wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (HAMAS) amesisitiza juu ya uhusiano mzuri wa harakati hiyo na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na kubainisha kwamba, HAMAS haikubaliani na ujeuri wa Washington katika kuamiliana na Tehran.
Mousa Mohammed Abu Marzook amebainisha kwamba, suala la kuiunga mkono Jamhuri ya Kiislamu ya Iran limejadiliwa katika safari yake huko nchini Russia na kuongeza kuwa, ili kukabiliana na vikwazo vya kidhalimu vya Marekani kuna haja ya kuwa pamoja na Iran.
Kiongozi huyo wa ngazi za juu wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (HAMAS) ameashiria nafasi ya Russia katika kufikiwa utatuzi wa kisiasa baina ya Palestina na Israel na kufikia mwisho nafasi ya Washington katika uwanja huo na kuongeza kwamba, Hamas haiwezi kuwa pamoja na utawala wa Kizayuni wa Israel ambao hautaki kuweko nchi huru ya Palestina mji mkuu ukiwa Quds au usiotaka kurejea wakimbizi wa Kipalestina katika ardhi zao.
Wiki hii, Mousa Mohammed Abu Marzook, alielekea Moscow Russia akiuongoza ujumbe wa ngazi za juu wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (HAMAS), ambapo akkiwa nchini humo malikutana na kufanya mazungumzo na viongozi mbalimbali akiwemo Mikhail Bogdanov, Naibu Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa nchi hiyo.