Arab League: Kuundwe mahakama maalumu ya jinai za Israel
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i5536-arab_league_kuundwe_mahakama_maalumu_ya_jinai_za_israel
Jumuiya ya Nchi za Kiarabu imetoa mwito wa kuundwa mahakama maalumu ya jinai kwa ajili ya kuwapandisha kizimbani Wazayuni kutokana na hatua yao ya kukiuka haki za Wapalestina.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Apr 21, 2016 10:52 UTC
  • Arab League: Kuundwe mahakama maalumu ya jinai za Israel

Jumuiya ya Nchi za Kiarabu imetoa mwito wa kuundwa mahakama maalumu ya jinai kwa ajili ya kuwapandisha kizimbani Wazayuni kutokana na hatua yao ya kukiuka haki za Wapalestina.

Akiongea mjini Cairo Misri katika mkutano wa dharura wa kujadili tamko la hivi karibuni la Benjamin Netanyahu, Waziri Mkuu wa utawala haramu wa Israel kuhusu eneo la miinuko ya Golan huko Syria, Nabil al-Arabi, Katibu Mkuu wa Arab League amesema, mienendo ya Tel Aviv inaashiria kuwa utawala huo haramu unajihisi uko juu ya sheria na hauwezi kuwajibishwa na yeyote.

Al-Arabi amesema, kuna haja ya kuundwa mahakama maalumu ya jinai kama ile ya jinai za kivita ya Serbia, ili utawala huo dhalimu utambue kuwa Mzayuni yeyote atakayekanyaga haki za Wapalestina ataandamwa na mkono wa sheria. Wajumbe kutoka nchi 22 wanachama wa Jumuiya ya Nchi za Kiarabu wanatazamiwa kupasisha azimio la kulaani tangazo la Netanyahu la Jumapili iliyopita, aliyejigamba kuwa utawala huo ghasibu hautairejesha miinuko ya Golan kwa Syria.

Hii ni katika hali ambayo, Mkuu wa sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya alisema kuwa, umoja huo hauutambui umiliki wa utawala wa Kizayuni wa Israel kwa miinuko ya Golan kwani eneo hilo ni ardhi ya Syria.

Federica Mogherini amesisitiza kuwa, Umoja wea Ulaya hautambui ukaliaji mabavu wa Israel dhidi ya ardhi za Palestina baada ya vita vya mwaka 1967 na kuongeza kuwa, huo ndio msimamo wa Umoja wa Ulaya na nchi wanachama wa umoja huo.