Ubunifu wa Ansarullah wa kuunda jopokazi la mapatano jumuishi ya kitaifa
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i55677-ubunifu_wa_ansarullah_wa_kuunda_jopokazi_la_mapatano_jumuishi_ya_kitaifa
Mahdi al-Mashat, Mkuu wa Baraza Kuu la Kisiasa la Yemen ametangaza kuwa, limeundwa jopokazi linalojumuisha shakhsia 20 wa nchi hiyo kwa madhumuni ya kuleta mapatano jumuishi ya kitaifa na kutatua kisiasa mgogoro unaoendelea nchini humo.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Aug 30, 2019 03:38 UTC
  • Ubunifu wa Ansarullah wa kuunda jopokazi la mapatano jumuishi ya kitaifa

Mahdi al-Mashat, Mkuu wa Baraza Kuu la Kisiasa la Yemen ametangaza kuwa, limeundwa jopokazi linalojumuisha shakhsia 20 wa nchi hiyo kwa madhumuni ya kuleta mapatano jumuishi ya kitaifa na kutatua kisiasa mgogoro unaoendelea nchini humo.

Hivi sasa Yemen inakabiliwa na hali mbaya zaidi kuwahi kushuhudiwa katika miongo mitatu ya karibuni. Kwa upande mmoja, nchi hiyo inakabiliana na vita vilivyoanzishwa na muungano wa kijeshi unaoongozwa na Saudi Arabia; na kwa upande mwingine inashuhudia vita vya miungano ya ndani, ambavyo kwa hakika ni vya baina ya Wayemeni wenyewe kwa wenyewe huko kusini mwa nchi. Wakati huo huo makundi ya kigaidi na hasa la Al Qaeda, limeyavamia na kuyakalia kwa mabavu baadhi ya maeneo ya nchi hiyo. Wakati serikali iliyojiuzulu ya Abdrabbuh Mansur Hadi iko kwenye hali ya kuyumba na kulegalega huko kusini mwa Yemen, serikali iliyoundwa na harakati ya Ansarullah na waitifaki wake katika mji mkuu wa nchi hiyo Sana'a, ina mshikamano, uthabiti na hali ya kuridhisha. Katika hali kama hiyo Mahdi al Mashat, Mkuu wa Baraza Kuu la Kisiasa la Yemen ametangaza habari ya kuundwa jopokazi la mapatano jumuishi ya kitaifa.

Mahdi al-Mashat, Mkuu wa Baraza Kuu la Kisiasa la Yemen

Hadi sasa hakuna taarifa yoyote iliyotolewa kuhusu wajumbe wa jopo hilo, lakini inavyoonekana, jopokazi hilo litajumuisha wadau na makundi mbali mbali ya kaskazini na kusini ya Yemen. Lengo muhimu zaidi la jopokazi hilo ni kulinda ardhi yote ya Yemen na kukabiliana na mpango na njama ambayo dhamira yake kuu ni hatimaye kuigawanya nchi hiyo na kuirejesha kwenye hali iliyokuwa nayo kabla ya mwaka 1990. Kuhusiana na nukta hiyo, Mahdi al Mashat amesema: "Muungano vamizi unatekeleza mikakati ya umwagaji damu katika maeneo ya kusini kupitia mpango wa kuimarisha ukaliaji wa mabavu na kuigawanya ardhi ya Yemen." Tariq Mustafa Salam, mkuu wa mkoa wa Aden na mjumbe wa jeshi la harakati ya malalamiko ya kusini mwa Yemen naye pia amesema: "Kinachotokea hivi sasa kusini mwa Yemen ni muendelezo wa kuigawanya Yemen na kuchochea mapigano na machafuko zaidi."

Mamluki wa Saudia na Imarati kusini mwa Yemen

Lakini mbali na hayo, Yemen hivi sasa ina hali inayoshabihiana na Libya, ambapo serikali kadhaa na makundi ya kigaidi na ya kikabila, kila moja linashikilia madaraka katika sehemu moja ya ardhi ya nchi hiyo, huku kukikosekana serikali kuu ya kitaifa. Kuundwa jopokazi lililotajwa kunaweza kusaidia kupatikana mwafaka baina ya wadau mbali mbali wa kisiasa nchini humo. Ukweli ni kwamba hatua hiyo iliyochukuliwa na Baraza Kuu la Kisiasa la Yemen inaonyesha kuwa, Ansarullah na waitifaki wake hawana nia ya kuhodhi madaraka na kuyapuuza makundi na wadau wengine hasa, makundi na mirengo ya kusini, bali wanachofuatilia ni kuunda serikali ya kitaifa itakayojumuisha na kushirikisha makundi yote ya nchi hiyo.

Lakini nukta nyingine ya tatu ni kuwa, kuundwa jopokazi kama hilo kunaweza kuwa sababu pia ya kupatikana mwafaka baina ya makundi yote ya Yemen wa kukabiliana na hujuma na mashambulio ya muungano vamizi wa Saudia; katika hali ambayo muungano huo hivi sasa hauna nguvu na hali kama uliyokuwa nayo huko nyuma, bali umedhoofika pia kutokana na tofauti na mivutano ya ndani. Kuundwa jopokazi hilo kunaweza pia kupunguza kasi ya maafa ya kibinadamu yanayoendelea kushuhudiwa hivi sasa nchini Yemen na kuzuia uporaji wa mali na utajiri wa kitaifa wa nchi hiyo. Imarati na Saudi Arabia kila moja inayashikilia baadhi ya maeneo ya ardhi ya Yemen, hususan bandari za nchi hiyo; ilhali nchi hiyo masikini ya Kiarabu hivi sasa inakabiliwa na hali mbaya sana ya kifedha na kibinadamu. Mahdi al Mashat anaizungumzia hali hiyo kwa kusema: "Vita na mapigano ndani ya muungano vamizi wa Saudia na Imarati kusini mwa Yemen ni sarakasi kubwa kubwa zaidi inayochezwa na wavamizi wa nchi hii ya Kiarabu, lengo lake kuu likiwa ni kuupora utajiri wake.".../