Mwanachama mwingine mwandamizi wa HAMAS amewekwa kizuizini nchini Saudi Arabia
(last modified Tue, 17 Sep 2019 08:12:45 GMT )
Sep 17, 2019 08:12 UTC
  • Mwanachama mwingine mwandamizi wa HAMAS amewekwa kizuizini nchini Saudi Arabia

Duru za Palestina zimetangaza kuwa mwanachama mwingine mwandamizi na muhimu wa Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Palestina (HAMAS) amekamatwa na kuwekwa kizuizini nchini Saudi Arabia.

Kwa mujibu wa duru hizo, Saudia imemkamata na kumweka kwenye jela ya wafungwa wa kisiasa ya Dhahban Abu Ubaidah Al Agha, mwana wa Khabri Al Agha, mmoja wa waasisi wa harakati ya Hamas.

Duru hizo zimebainisha kuwa, Abu Ubaidah al Agha ni miongoni mwa viongozi wa Hamas walioko nchini Saudi Arabia, ambaye ana uraia wa nchi hiyo; na hakuna sababu yoyote iliyotolewa kuhusiana na yeye kuendelea kuwekwa kizuizini.

Muhsin Saleh, mkuu wa kituo cha utafiti cha Az-Zaitunah amesema, maafisa wa Saudia wamemkamata na kumweka kizuizini al Agha kwa zaidi ya mwaka mmoja na nusu sasa na akaongeza kuwa, utawala wa Aal Saud umewakamata na kuwafunga jela Wapalestina wapatao 60 bila kuwabainishia makosa waliyofanya wala mashtaka yanayowakabili.

Wiki iliyopita, harakati ya Hamas ilitoa taarifa kuhusiana na kukamatwa na kuwekwa kizuizini Muhammad al Khidhri, kiongozi mwandamizi wa harakati hiyo, ambaye anashikiliwa kwa miezi kadhaa sasa na mamlaka za Saudia na ikataka aachiliwe huru.../

Tags