Hamas: Mbinu zote zinazowezekana zitumike katika kulinda Msikiti wa Al Aqsa
Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (Hamas) imetoa wito wa kutumiwa kila mbinu inayowezekana katika kuulinda na kuutetea Msikiti wa Al Aqsa ulio katika mji wa Quds (Jerusalem) unaokaliwa kwa mabavu na utawala haramu wa Israel.
Mkuu wa Idara ya Kimataifa ya Habari katika harakati ya Hamas Rafat Murra amesisitiza kuhusu kutumiwa kila mbinu inayowezekana kukabiliana na utawala ghasibu wa Israel na walowezi magaidi wa Kizayuni.
Aidha amesisitiza kuhusu umuhimu wa kidini wa Msikiti wa Al Aqsa na nafasi muhimu ya msikiti huo miongoni mwa Wapalestina na Umma wa Kiislamu na kuongeza kuwa: "Taarifa zinadokeza kuwa, utawala wa Kizayuni unatekeleza njama ya kuanzisha wimbi jipya la kuuhujumu msikiti wa Al Aqsa katika siku na wiki zijazo."
Mwanachama huyu mwandamizi wa Hamas amesisitiza kuwa, harakati hiyo itaendeleza mapambano yake ya kujitolea kulinda matukufu ya Kiislamu na kuvunja njama zote za utawala wa Kizayuni wa Israel.
Oktoba mwaka 2017 Shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni la Umoja wa Mataifa (UNESCO) lilitangaza rasmi kuwa Msikiti wa al Aqsa mjini Quds ni wa Waislamu na kwamba Mayahudi hawahusiki kivyovyote vile na msikiti huo.
Pamoja na hayo wanajeshi wa utawala wa Kizayuni wa Israel na walowezi wa Kizayuni huuhujumu msikiti huo mara kwa mara na kuuvunjia heshima ikiwa ni katika jitihada za kufuta turathi hiyo ya Kiislamu.