Saudi Arabia yavunja rekodi yake ya kunyonga watu
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i56469-saudi_arabia_yavunja_rekodi_yake_ya_kunyonga_watu
Katika kipindi cha miezi 9 iliyopita ya mwaka huu wa 2019, Saudi Arabia imeshatekeleza adhabu ya kifo kwa watu 160 na kuvunja rekodi yake ya huko nyuma ya kutekeleza adhabu hiyo kwa watu wengi zaidi duniani.
(last modified 2025-11-19T02:13:06+00:00 )
Oct 07, 2019 07:55 UTC
  • Saudi Arabia yavunja rekodi yake ya kunyonga watu

Katika kipindi cha miezi 9 iliyopita ya mwaka huu wa 2019, Saudi Arabia imeshatekeleza adhabu ya kifo kwa watu 160 na kuvunja rekodi yake ya huko nyuma ya kutekeleza adhabu hiyo kwa watu wengi zaidi duniani.

Kwa mujibu wa Shirika la Kimataifa la Haki za Binadamu la Amnesty International, mwaka jana yaani 2018, Saudi Arabia ilitekeleza adhabu ya kifo kwa watu 149.

Idadi ya watu wanaotekelezewa adhabu ya kifo nchini Saudia imeongezeka sana katika miaka ya hivi karibuni kiasi kwamba rekodi ya kuuliwa watu 70 ya mwaka 2013 nchini humo hivi sasa imepanda na kufikia watu 160 katika kipindi cha miezi tisa tu ya mwaka huu, ikiwa imebakia miezi mingine mitatu hadi kumalizika mwaka 2019. Hivi sasa kuna hatari ya kutekelezewa adhabu ya kifo watu wengine 39 nchini Saudi Arabia akiwemo mtoto mmoja mdogo anayejulikana kwa jina la Ali al Nimr.

Baadhi ya masheikh wa Saudi Arabia wanaosubiri kutekelezewa adhabu ya kukatwa vichwa kutokana na kuukosoa utawala wa Saudi Arabia

 

Hadi hivi sasa ukoo wa Aal Saud unaendelea kukataa kukabidhi kwa familia zao miili ya watu 83 iliowatekelezea adhabu ya kifo mwaka 2016 ukiwemo mwili wa shahid Sheikh Baqir Muhammad Baqir al Nimr aliyeuliwa kidhulma na utawala wa Saudi Arabia.

Taasisi ya Haki za Binadamu ya Saudia yenye makao yake barani Ulaya imesema kuwa, idadi ya watu waliotekelezewa adhabu ya kifo katika kipindi cha miezi sita ya mwanzo ya mwaka huu wa 2019 huko Saudi Arabia haijawahi kushuhudiwa katika kipindi cha miaka mitano iliyopita. Kwa mujibu wa taasisi hiyo, mwaka jana 2018, idadi ya watu waliotekelezewa adhabu ya kifo huko Saudia ilikuwa ni watu 55 katika kipindi cha miezi sita ya awali ya mwaka huo, lakini katika kipindi kama hicho mwaka huu, idadi hiyo imeongezeka zaidi ya mara mbili na kufikia watu 122.