Israel yakiri kuwaua kigaidi viongozi wa HAMAS nje ya Palestina
(last modified Sat, 12 Oct 2019 02:31:30 GMT )
Oct 12, 2019 02:31 UTC
  • Israel yakiri kuwaua kigaidi viongozi wa HAMAS nje ya Palestina

Mkuu wa Shirika la Kijasusi la utawala wa Kizayuni MOSSAD amekiri kuwa, utawala huo dhalimu umekuwa ukiwaandamana na kuwaua kigaidi viongozi wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS nje ya ardhi hizo zinazokaliwa kwa mabavu na Wazayuni.

Kituo cha Upashaji Habari cha Palestina kimemnukuu mkuu huyo wa Mossad, Yossi Cohen akikiri hivyo jana na kuongeza kuwa, Fadi Mohammad al Batsh mhandisi mahiri na stadi ambaye pia alikuwa mmoja wa viongozi wa HAMAS aliuliwa kigaidi mwaka jana na majasusi wa Mossad nchini Malaysia.

Mwaka jana watu wasiojulikana walimuua kigaidi mhandisi al Batsh nchini Malaysia na mara baada ya mauaji hayo, Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS ilisema kuwa kulingana na ushahidi ilio nao, ugaidi huo ulifanywa na shirika la kijasusi la Israel, MOSSAD.

Katika upande mwingine, ushahidi wa kuaminika unaonesha kuwa, kiongozi mwingine wa HAMAS, Mahmoud al Mabhouh naye aliuliwa kigaidi na genge la mauaji la Mossad akiwa Umoja wa Falme za Kiarabu, kama ambavyo shirika hilo la mauaji la kigaidi la Israel lilimuua pia kigaidi msomi mwingine wa HAMAS, mhandisi Mohamed Zouari nchini Tunisia.

Hadi hivi sasa utawala wa Kizayuni wa Israel umeshafanya mauaji mengi ya kigaidi dhidi ya viongozi wa makundi ya muqawama likiwemo lile la HAMAS.

Hivi karibuni utawala katili wa Israel ulitoa orodha mpya ya viongozi wa HAMAS wanaopaswa kuuliwa kigaidi huku mkuu wa Brigedi za Izuddin al Qassam, tawi la kijeshi la harakati hiyo na kaimu wake wakiwa juu kabisa ya orodha hiyo ya Israel.

Tags