Arab League: Operesheni ya Uturuki nchini Syria ni uvamizi wa kijeshi
(last modified Sun, 13 Oct 2019 07:55:28 GMT )
Oct 13, 2019 07:55 UTC
  • Arab League: Operesheni ya Uturuki nchini Syria ni uvamizi wa kijeshi

Jumuiya ya Nchi za Kiarabu imesema operesheni inayofanywa na vikosi vya jeshi la Uturuki huko kaskazini mwa Syria ni uvamizi wa wazi wa kijeshi.

Katibu Mkuu wa Arab League, Ahmed Aboul-Gheit amesema hayo katika kikao cha dharura cha mawaziri wa mambo ya nje wa nchi wanachama wa jumuiya hiyo kilichoanza jana Jumamosi mjini Cairo, Misri na kusisitiza kuwa, serikali ya Ankara inapaswa kusitisha operesheni hiyo mara moja.

Amebainisha kuwa, "Kile ambacho Uturuki inakifanya nchini Syria ni jinai za kivita na dhidi ya binadamu. Operesheni hiyo ya kijeshi haina uhalali wa kimataifa."

Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Nchi za Kiarabu ameonya kuwa, yumkini idadi ya watu wanaolazimika kukimbia makazi yao kutokana na operesheni hiyo huko kaskazini mwa Syria ikapindukia watu 300,000.

Operesheni ya Uturuki dhidi ya wapiganaji wa Kikurdi nchini Syria

Ahmed Aboul-Gheit ameongeza kuwa, hana chembe ya shaka kuwa operesheni hiyo ya Uturuki dhidi ya Syria itavuruga usalama na uthabiti katika eneo zima.

Licha ya taasisi nyingi za kimataifa kutahadharisha kuhusu taathira hasi za mashambulizi hayo, lakini Rais Recep Tayyep Erdogan wa Uturuki anasisitiza kuwa, operesheni hiyo ya kijeshi ya nchi yake kwa jina la "Chemchemi ya Amani" dhidi ya wapiganaji wa Kikurdi huko kaskazini mwa Syria itaendelea.