Wazayuni wazidi kuwanyanyasa Wapalestina, wamtia mbaroni mkuu wa mkoa
Wanajeshi wa utawala wa Kizayuni wa Israel wameendeleza unyanyasaji wao dhidi ya Wapalestina kwa kumtia mbaroni mkuu wa mkoa wa Quds na viongozi wengine wa harakati ya Fat'h katika Ukingo wa Magharibi wa Mto wa Mto Jordan.
Jana Jumatatu, wanajeshi katili wa Israel walivamia nyumba ya Mkuu wa Mkoa wa Quds, Adnan Gheith katika mji wa Silwan na kumuweka chini ya ulinzi.
Wanajeshi hao wa Israel wamemtia mbaroni pia Katibu Mkuu wa Fat'h katika mji wa Quds, Shadi Mutawwar pamoja na Yaser Darwish, Katibu Mkuu wa harakati hiyo katika eneo la Isawiya.
Kamati ya Palestina Masuala ya Mateka na Wakimbizi imelaani vikali kutiwa mbaroni mara kwa mara mkuu wa mkoa wa Quds na Katibu Mkuu wa harakati ya Fat'h katika mkoa huo.
Itakumbukkwa kuwa, mwanzoni mwa mwezi huu wa Oktoba pia, wanajeshi dhalimu wa utawala wa Kizayuni walimtia mbaroni Waziri wa Masuala ya Quds wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina pamoja na maafisa wengine sita wa serikali hiyo inayoongozwa na Mahmoud Abbas.
Kila siku Wazayuni wanashambulia na kuvamia maeneo mbalimbali ya Wapalestina kwa madai ya kipuuzi, huku shabaha yao kuu ikiwa ni kufanikisha malengo yao haramu katika ardhi wanazozikalia kwa mabavu za Palestina.
Jopo la kufuatilia masuala ya mateka wa Palestina limesema katika ripoti yake maalumu kuwa, Wapalestina waliotekwa nyara na ambao hivi sasa wanashikiliwa na utawala wa Kizayuni katika korokoro za kuogofya ni 6,500. Kati ya mateka hao, 230 ni watoto wadogo; wanawake ni karibu 50, mateka wanaoshikiliwa bila ya kufunguliwa mashtaka ni 500 huku 800 wengine wakiwa ni wagonjwa wanaohitajia huduma maalumu za matibabu.