Qatar: Diplomasia itumike kupunguza taharuki kati ya Iran na Waarabu
Msemaji wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Qatar amesema Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na baadhi ya nchi za Kiarabu katika eneo zinaweza kupunguza taharuki miongoni mwao kwa njia ya mazungumzo na diplomasia.
Lolwah al-Khater amesema taharuki iliyopo haijasababishwa na migawanyiko ya kimadhehebu kama wengi wanavyodhani, bali imechochewa na mashindano ya kugombania ubabe na ushawishi katika eneo.
Amesisitiza kuwa, migogoro katika eneo la Asia Magharibi inaweza kupatiwa ufumbuzi na nchi za eneo kwa kutoa kipaumbele kwa maslahi yao ya pamoja, badala ya kugetemea nchi ajinabi.
Matamshi ya al-Khater yamekuja siku chache baada ya Naibu Waziri Mkuu ambaye pia ni Waziri wa Mambo ya Nje wa Qatar, Sheikh Mohammed bin Abdulrahman Aal-Thani kusisitiza kuwa Doha inakaribisha kustawishwa uhusiano na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika nyanja zote.
Alisema kuwa uhusiano wa Tehran na Doha ni wa kirafiki, kidugu na unaopiga hatua; na kusisitiza kuwa uhusiano wa nchi mbili hizi rafiki unapasa kuendelezwa katika nyanja zote zikiwemo za kisiasa, kiuchumi na kiutamaduni.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Qatar alieleza bayana kuwa, "Iran na Qatar zinatofautiana katika baadhi ya mambo, lakini hilo halijavuruga uhusiano na maelewano yetu katika mambo mengine, sote tukifahamu fika kuwa sisi ni majirani na tunahitajiana."