Kuanza uchunguzi kuhusu ufisadi wa kifedha Lebanon
Rais Michel Aoun wa Lebanon ametangaza kuwa wiki ijayo mafaili ya ufisadi wa kifedha yatafikishwa katika mahakama za nchi hiyo kwa ajili ya uchunguzi.
Kuanzia 17 Oktoba Lebanon imekuwa ikishuhudia maandamano ya wananchi. Ingawa Saad Al Hariri amejiuzulu kama waziri mkuu wa Lebanon, lakini maandamano ya wananchi yangali yanaendelea. Moja ya sababu kuu za maandamano ya watu wa Lebanon ni ufisadi mkubwa nchini humo hasa ufisadi wa kifedha.
Lebanon inakumbwa na matatizo makubwa ya kisiasa ikiwa ni pamoja na deni la dola bilioni 86, ukosefu wa ajira ambao kiwango chake kinakaribia asilimia 35 miongoni mwa vijana na kuongezeka umasikini nchini humo.
Kile ambacho watu wa Lebanon wanalalamikia ni kuwa, kwa nini wananchi wa kawaida wabebeshwe mzigo wote wa matatizo ya kiuchumi huku baadhi ya wanasiasa ambao wamehusishwa na ufisadi wa mabilioni ya dola wakiweka fedha walizoiba katika akaunti zao binafsi nje ya nchi.
Cheche za maandamano ya sasa Lebanon zilianzishwa na uamuzi wa serikali kuweka ushuru kwa ajili ya mawasiliano ya njia ya mitandao ya kijamii.
Mapambano dhidi ya ufisadi ni jambo muhimu sana kwa watu wa Lebanon kiasi kwamba Muungano wa Muqawama katika uchaguzi wa bunge Mei 2018 ulitangaza kauli mbiu yake kuu kuwa ni vita dhidi ya ufisadi. Kuchaguliwa nara hiyo kulikuwa na maana ya kutambua matatizo ya Lebanon na ufahamu wa juu wa Hizbullah na waitifaki wake kuhusu matakwa ya wananchi.
Nara ya vita dhidi ya ufisadi ilikuwa moja ya sababu za ushindi mkubwa wa Muungano wa Muqawama katika uchaguzi wa bunge Lebanon mwaka jana ambapo muungano huo ulipata viti 68 kati ya viti 128 vya bunge.
Kwa msingi huo, baada ya Saad al Hariri kuunda baraza la mawaziri, Hizbullah na waitifaki wake walitangaza vita dhidi ya ufisadi kuwa takwa lao muhimu zaidi.
Pamoja na hayo, mfumo wa ugavi wa madaraka nchini Lebanon umetajwa kuwa moja sababu kuu za kuenea ufisadi nchini humo. Kimsingi ni kuwa, mfumo huo wa ugavi wa madaraka umezuia kuundwa serikali ya waliowengi Lebanon na hivyo kuandaa mazingira ya wanasiasa kutumia vibaya madaraka. Aidha kutumia vibaya tafauti za kidini, kimadhehebu na kikaumu ni sababu nyingine ya kuenea ufisadi katika nchi hiyo ya Kiarabu yenye idadi ya watu takribani milioni sita.
Hali kadhalika mfumo wa ugavi wa madaraka nchini Lebanon ni sababu ambayo hupelekea kuahirishwa kwa muda mrefu uundwaji wa serikali nchini humo na hivyo kuongeza muda ambao nchi hiyo hukaa bila serikali. Nukt hiyo ni chanzo cha maslahi ya kimrengo au kikaumu kuwekwa mbele ya maslahi ya kitaifa.
Kuendelea maandamano ya wananchi wa Lebanon kumepelekea viongozi wa nchi hiyo kutangaza vita dhidi ya mafisadi ambao aghalabu ni wanasiasa wa sasa na wa zamani.
Michel Aoun, Rais wa Lebanon, siku ya Alhamisi aligusia nukta hiyo na kusema baadhi ya viongozi au wanasiasa wa sasa na wa zamani wa Lebanon ambao ni washukiwa wa ufisadi wa kifedha wataanza kusailiwa bila kujali nyadhifa zao. Aidha alisema kuwa, serikali ijayo ya Lebanon itaundwa na mawaziri wanaostahiki na ambao hawakabiliwi na tuhuma za ufisadi.
Iwapo wakuu wa Lebanon wataweza kukabiliana na ufisadi ipasavyo basi wataweza kurejesha imani ya wananchi iliyotoweka na kwa msingi huo kuandaa mazingira ya kuwepo serikali yenye kutenda kazi kwa maslahi ya taifa.
Nukta nyingine muhimu ya kutatua mgogoro wa sasa na vita dhidi ya ufisadi Lebanon ni kuwa hakupaswi kuwa na uingilaji wa ajinabi katika maambo ya ndani ya nchi hiyo hasa katika kuundwa serikali.