Hamas: Masjidul Aqsa ni mstari mwekundu usiopaswa kuguswa
(last modified Wed, 11 Dec 2019 08:04:16 GMT )
Dec 11, 2019 08:04 UTC
  • Hamas: Masjidul Aqsa ni mstari mwekundu usiopaswa kuguswa

Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (HAMAS) imetahadharisha kuhusu vitendo vya walowezi wa Kizayuni vya kuendelea kuuvunjia heshima Msikiti wa al Aqsa huko Palestina inayokaliwa kwa mabavu.

Taarifa iliyotolewa na Hamas imesema kuwa, kuhujumu na kuvunjia heshima Msikiti wa al Aqsa ni sawa na kucheza na moto. Taarifa hiyo imeongeza kuwa, njama za utawala wa Kizayuni wa Israel za kutaka kulazimisha matakwa yake kuhusiana na Msikiti wa Alqsa hazitazaa matunda na Intifadha na mapambano ya wakazi wote wa Quds ni ujumbe wa wazi kwa viongozi wa utawala ghasibu wa Israel.

Harakati ya Hamas pia imewapongeza wakazi wa mji wa Quds kwa kuulinda Msikiti wa al Aqsa na maeneo mengine matakatifu na kusisitiza kuwa, Quds na Msikiti wa al Aqsa ni maeneo ya Kiislamu, na taifa la Palestina litaendelea kutetea na kuyalinda maeneo hayo. 

Askari wa Israel wakivamia Msikiti wa al Aqsa

Hamas pia imeitaka Jumuiya ya Nchi za Kiarabu kukabiliana na uhalifu wa wazayuni wa Israel dhidi ya Msikiti wa al Aqsa. 

Msikiti huo na maeneo mengine matukufu ya Kiislamu vimekuwa vikishambuliwa na kuvunjiwa heshima mara kwa mara na Wazayuni wa Israel wanaopewa himaya na jeshi la utawala huo.    

Tags