Bahrain yamkosoa Amir wa Qatar kwa kutohudhuria kikao cha Riyadh
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i57813-bahrain_yamkosoa_amir_wa_qatar_kwa_kutohudhuria_kikao_cha_riyadh
Waziri wa Mambo ya Nje wa Bahrain ameitaja hatua ya Amir wa Qatar ya kutoshiriki kikao cha wakuu wa nchi wanachama wa Baraza la ushirikiano la Ghuba ya Uajemi huko Riyadh Saudi Arabia kuwa ni ishara ya kutokuwa na azma Doha ya kuhitimisha mgogoro baina yake na nchi nne za Kiarabu.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Dec 11, 2019 09:04 UTC
  • Bahrain yamkosoa Amir wa Qatar kwa kutohudhuria kikao cha Riyadh

Waziri wa Mambo ya Nje wa Bahrain ameitaja hatua ya Amir wa Qatar ya kutoshiriki kikao cha wakuu wa nchi wanachama wa Baraza la ushirikiano la Ghuba ya Uajemi huko Riyadh Saudi Arabia kuwa ni ishara ya kutokuwa na azma Doha ya kuhitimisha mgogoro baina yake na nchi nne za Kiarabu.

Kikao cha nne cha Baraza la Ushirikiano la Ghuba ya Uajemi kilifanyika jana huko Riyadh mji mkuu wa Saudi Arabia bila ya kuhudhuriwa na Sheikh Tamim bin Hamad Al Thani Amir wa Qatar ambaye alialikwa na Mfalme wa Saudi Arabia. 

Amir wa Qatar, Sheikh Tamim bin Hamad Al Thani 

Badala yake Amir wa Qatar  alimtuma Sheikh Abdallah bin Nasir bin Khalifa Al Thani Waziri Mkuu wa nchi hiyo katika kikao hicho. Khalid bin Ahmad Waziri wa Mambo ya Nje wa Bahrain amesema katika radiamali yake kwa hatua hiyo ya Qatar kuwa: Bahrain inaheshimu mitazamo na maombi yaliyofikiwa katika kikao cha Cairo Julai Tano mwaka juzi. 

Naye Anwar Gargash Waziri Mshauri katika masuala ya nje wa Umoja wa Falme za Kiarabu (Imarati) amejibu hatua ya Amir wa Qatar ya kutoshiriki kikao cha Riyadh kwa kusema: Mgogoro kati ya nchi za Kiarabu za pambizoni mwa Ghuba ya Uajemi ungali unaendelea. 

Saudi Arabia, Imarati, Bahrain na Misri Julai 5 mwaka juzi ziliituhumu Qatar kuwa inaunga mkono ugaidi na kisha zikakata uhusiano na nchi hiyo na kuifungia Doha mipaka ya nchi kavu, baharini na angani. 

Si hayo tu bali nchi hizo nne za Kiarabu ziliipatia Qatar masharti 13 kama inataka kuhuisha uhusiano na nchi hizo hata hivyo Doha iliyapinga masharti hayo na kuyataja kuwa yanakiuka haki yake ya kujitawala.