Oman na Qatar zataka kuimarisha uhusiano na Iran
(last modified Sun, 15 Dec 2019 08:01:32 GMT )
Dec 15, 2019 08:01 UTC
  • Oman na Qatar zataka kuimarisha uhusiano na Iran

Spika wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu (Bunge la Iran) amesema taifa hili linajivunia kuwa na uhusiano mzuri na wa udugu na Oman huku akisisitizia umuhimu wa kuimarishwa uhusiano huo.

Dakta Ali Larijani amesema hayo katika mazungumzo yake na Khalid bin Hilal Al Mawali, Mwenyekiti wa Baraza la Shura la Oman pambizoni mwa Mkutano wa 12 wa Jumuiya ya Mabunge ya Asia nchini Uturuki na kuongeza kuwa, "Nina matumaini kuwa makubaliano ya pande mbili ya Kamisheni ya Pamoja ya Uchumi ya Oman na Iran yataanza kuzaa matunda hivi karibuni kutokana na jitihada zinazofanywa na wafanyabiashara na wajasiriamali wa nchi mbili hizi."

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Baraza la Shura la Oman amesema, "Bila shaka Iran ni nchi ya kistaratajia katika eneo, na ina uwezo na nafasi ya kipekee katika nyuga za siasa na uchumi."

Mapema leo, Spika wa Bunge la Iran alikutana na kufanya mazunugumzo pia na mwenzake wa Qatar, Ahmad bin Abdullah al-Mahmoud ambapo wamebadilishana mawazo kuhusu uhusiano wa pande mbili, masuala ya kieneo na kimataifa.

Dakta Larijani ameipongeza Qatar kwa kusimama kidete dhidi ya vikwazo ilivyowekewa na Saudia na waitifaki wake, na kueleza bayana kuwa, Jamhuri ya Kiislamu ina hamu ya kuona uhusiano wa Doha na Tehran unaimarika zaidi katika nyuga mbali mbali hususan uga wa uchumi.

Spika Larijani akihutubia  Mkutano wa 12 wa Jumuiya ya Mabunge ya Asia nchini Uturuki

Naye Ahmad bin Abdullah al-Mahmoud, Spika wa Bunge la Qatar amesema Iran ni ndugu na jirani mwenye muamana, kwani ilisimama na Qatar wakati viliposhadidi vikwazo dhidi yake.

Amesema serikali ya Doha itaendelea kupinga masharti 13 iliyopewa na Baraza la Ushirikiano la Ghuba ya Uajemi ili iondolewa vikwazo. Kadhalika amekosoa vikali dhulma zinazofanywa na utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya Wapalestina, na kusisitiza kuwa Wapalestina wenyewe wana haki ya kuamua mustakabali wao.

Tags