Hamas: Utawala wa Kizayuni ndio utakaobeba dhima ya lolote litakalotokea + Video
(last modified Thu, 26 Dec 2019 11:53:23 GMT )
Dec 26, 2019 11:53 UTC
  • Hamas: Utawala wa Kizayuni ndio utakaobeba dhima ya lolote litakalotokea + Video

Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS imesema kuwa, utawala wa Kizayuni ndio utakaobeba dhima ya lolote litakalotokea kutokana na mashambulizi yake ya mara kwa mara katika Ukanda wa Ghaza.

Televisheni ya al Alam imetangaza habari hiyo leo na kumnukuu msemaji wa HAMAS, Fawzi Barhum, akisema kuwa, mashambulizi ya hivi karibuni ya utawala wa Kizayuni ni njama za kuhamisha migogoro ya ndani ya Israel na kuipeleka nje ya utawala huo dhalimu. Ameongeza kuwa, mashambulizi hayo mapya ya utawala wa Kizayuni yanaonesha jinsi Israel ilivyozama kwenye lindi la kina kirefu la migogoro ya ndani.

Amesema, utawala wa Kizayuni umefeli katika milingano mipya ya taarifa za kijasusi na kijeshi za brigedi za Izzuddin. Ameongeza kuwa, utawala wa Kizayuni haujui madhara utakayopata kutokana na uchokozi wake lakini unapaswa kutambua kuwa adui hawezi kuubebesha muqawama wa Palestina milingano mipya.

Mapema leo asubuhi, utawala wa Kizayuni wa Israel umeshambulia eneo la Beit Lahia la kaskazini mwa Ukanda wa Ghaza.

 
Habari nyingine zinasema kuwa, Avigdor Lieberman, waziri wa zamani wa vita wa Israel amesema kuhusu mkanda wa video uliosambazwa jana Jumatano na vyombo vya habari unaomuonesha waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu akikimbia mashambulizi ya wanamapambano wa Palestina akiwa katika kitongoji cha walowezi wa Kizayuni cha Asqalan kwamba, kitendo hicho cha Netanyahu kinaonesha udhaifu wa Israel na kupoteza nguvu zake za kuzuia mashambulizi.

Lawama dhidi ya Netanyahu zimeongezeka sana baada ya kusambazwa mkanda huo wa video unaoonesha jinsi waziri mkuu huyo wa Israel anavyoogopa kifo.

Tags