Hamas: Hatutaruhusu Mpango wa ‘Muamala wa Karne” utekelezwe
Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS imetangaza kuwa, katu haitaruhusu mpango uliojaa njama wa Marekani-Israel wa Muamala wa Karne utekelezwe na kufikia malengo yake machafu.
Katika radiamali yake kwa kuweko taarifa za kuzinduliwa mpango wa Marekani na Israel wa Muamala wa Karne katika siku za usoni, Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS imetangaza kuwa, harakati hiyo haitaruhusu kutekelezwa mpango wowote ule ambao ni utangulizi wa kukanyagwa haki za Wapalestina.
Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS imesisitiza kuwa, wananchi wa Palestina ndio watakaoamua hatima na mustakabali wa taifa lao na si vinginevyo.
Karibuni hivi, Rais Mahmoud Abbas wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina alinukuliwa akitangaza bayana kwamba, Wapalestina wataendeleza upinzani wao dhidi ya mpango wa Marekani wa "Muamala wa Karne" na katu hawawezi kuutambua mpango huo uliojaa njama dhidi ya taifa la Palestina.
Muamala wa Karne ni mpango mpya uliopendekezwa na Marekani wenye lengo la kufutilia mbali haki za raia wa Palestina. Mpango huu umeandaliwa kwa kushirikiana na kufikiwa mapatano baadhi ya nchi za Kiarabu zikiwemo Saudi Arabia, Bahrain na Imarati.
Kwa mujibu wa mpango huo wa Marekani, Quds Tukufu itakabidhiwa kwa utawala wa Kizayuni; wakimbizi wa Kipalestina hawatakuwa na haki tena ya kurejea katika ardhi za mababu zao na Palestina itamiliki tu ardhi zitakazosalia huko katika Ukingo wa Magharibi mwa Mto Jordan na Ukanda wa Gaza.