Palestina yaomba kikao cha dharura cha Jumuiya ya Nchi za Kiarabu
Mamlaka ya Ndani ya Palestina (PA) imeomba kikao cha dharura cha Jumuiya ya Nchi za Kiarabu baada ya kuzinduliwa kile ambacho Marekani imekitaja kuwa 'Muamala wa Karne' kuhusu kadhia ya Palestina.
Mamlaka ya Ndani ya Palestina imetaka kikao cha dharura cha Jumuiya ya Nchi za Kiarabu kifanyike katika kiwango cha mawaziri wa mambo ya nje ili kujadili taathira za 'Maumala wa Karne'.
Kuhusiana na maudhui hiyo, Azzam al-Ahmad, mwanachama wa ngazi za juu wa Harakati ya Ukombozi wa Palestina (PLO) ametangaza kuwa, Mamlaka ya Ndani ya Palestina katu haitaafiki 'Muamala wa Karne' kutokana na kuwa ni muamala wa upande mmoja.
Mpango wa Muamala wa Karne uliopendekezwa na Marekani unajumuisha kukabidhiwa kikamilifu Israel mji mtakatifu wa Quds wenye Kibla cha Kwanza cha Waislamu yaani Msikiti wa al Aqsa, vitongoji vilivyoko katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan vyote vipewe Israel na Wapalestina wasiwe na haki ya kurejea kwenye ardhi za mababu zao.
Mpango huo batili ambao Rais wa Marekani, Donald Trump ameuzindua Jumanne mbele ya Waziri Mkuu wa utawala wa Kizayuni, Benjamin Netanyahu umepingwa vikali na ulimwengu wa Kiislamu na Kiarabu na hata Wapalestina wenyewe.