Kukombolewa Khan Tuman; ushindi muhimu nchini Syria
Vikosi vya jeshi la Syria vimelikomboa eneo la Khan Tuman katika operesheni za kuyatimua makundi ya kigaidi katika maeneo ya nchi hiyo yaliyokuwa yamevamiwa na kukaliwa kwa mabavu na makundi hayo.
Eneo la Khan Tuman liko kusini magharibi mwa mji wa Aleppo (Halab). Eneo hilo lilikombolewa mwezi Desemba mwaka 2015 kutoka kwenye makucha ya makundi ya kigaidi. Mwezi Machi mwaka 2016 magaidi wa kundi la Jabhatu-Nusrah, wakishirikiana na makundi mengine kadhaa ya kigaidi walijaribu tena kulishamulia eneo la Khan Tuman, lakini shambulio hilo lilizimwa na jeshi la Syria likisaidiwa na Hizbullah ya Lebanon, wapiganaji wa Fatimiyyun, vikosi vya muqawama vya Iraq na vikosi maalumu vya washauri wa kijeshi wa Iran. Magaidi wa An-Nusrah na wa megenge mengine ya kigaidi walilazimika kurudi nyuma baada ya wapiganaji wao mia minne kuangamizwa.
Mnamo mwezi Mei 2016, magaidi wa Jabhatu-Nusrah walikishambulia tena kitongoji cha Khan Tuman na kufanikiwa kulidhibiti na kulikalia kwa mabavu eneo hilo muhimu. Hata hivyo baada ya kukaliwa kwa mabavu na kundi hilo la kigaidi kwa muda wa takribani miaka minne, hivi sasa Khan Tuman imekombolewa tena.
Suali muhimu linaloulizwa hapa ni, kwa nini magaidi wamekuwa wakipigania sana kulivamia na kulidhibiti eneo la Khan Tuman; na je, kukombolewa kitongoji hicho kutakuwa na faida na manufaa gani kwa jeshi la Syria na waitifaki wake?
Sababu ya kwanza ya umuhimu wa kitongoji cha Khan Tuman inahusu nafasi yake ya kijiografia. Kitongoji hicho kiko umbali wa kilomita 10 had 14 kusini mwa mji wa Aleppo na karibu na barabara kuu itokayo Aleppo kuelekea Damascus, mji mkuu wa Syria. Kwa sababu hiyo, kitongoji cha Khan Tuman kina umuhimu wa kistratejia, kwa sababu kingewawezesha magaidi kuufikia mji muhimu wa Aleppo na pia kupanua harakati zao hadi mji mkuu Damascus.
Sababu nyingine ya umuhimu wa kukombolewa Khan Tuman ni kwamba, kitongoji hicho cha kistratejia kilikuwa moja ya njia kuu za kufikishiana misaada magaidi kutoka kaskazini hadi kusini mwa mkoa wa Aleppo. Kudhibitiwa kitongoji hicho na jeshi la Syria kwa ushirikiano na vikosi vya muqawama, kutafunga moja ya njia muhimu za mawasiliano za makundi ya kigaidi kutoka kaskazini hadi katikati ya Syria. Wakati huohuo, kukombolewa kitongoji hicho kutaliwezesha jeshi la Syria pamoja na waitifaki wake kutuma kwa wepesi na urahisi zaidi misaada na askari wa kuongeza nguvu kwa vikosi vyao vilivyoko kwenye mikoa ya Aleppo, Homs, Hama na Damascus.
Sababu ya tatu ya umuhimu wa kukombolewa Khan Tuman ni kuandaa mazingira ya kuendelezwa ushindi dhidi ya magaidi katika medani zingine. Ukweli ni kwamba kukombolewa Khan Tuman kutafunga njia za mawasiliano za magidi na kufungua njia za ufikishaji misaada na askari wa kuongeza nguvu kwa jeshi la Syria na waitifaki wake na hivyo kuwezesha kupatikana ushindi dhidi ya magaidi katika medani zingine.
Yote hayo ndiyo yaliyoifanya Saudi Arabia na Uturuki, wakati Khan Tuman ilipokombolewa kutoka kwenye makucha ya magaidi Desemba 2015, ziamue kukiuka usitishaji vita na kuyasaidia makundi ya kigaidi na hasa la Jabhatu-Nusrah ili liweze kulivamia na kulikalia tena kwa mabavu eneo hilo. Wakati eneo la Khan Tuman lilipokaliwa tena na kundi la kigaidi la Jabhatu-Nusrah mwaka 2016, Muladh Miqdad, mtaalamu wa masuala ya kijeshi wa Syria alisema, sababu pekee iliyopelekea kukaliwa tena kwa mabavu eneo hilo ni jeshi la Syria kuheshimu usitishaji vita na magaidi na waungaji mkono wao kuitumia fursa hiyo kuivamia na kuikalia kwa mabavu tena Khan Tuman. Kwa hiyo tunaweza kusema, sababu ya nne ya umuhimu wa kukombolewa kitongoji cha Khan Tuman ni kwamba, ushindi na mafanikio hayo ni pigo muhimu kwa waungaji mkono wa magaidi hususan Uturuki na Saudia.
Na sababu ya tano ya umuhimu wa kukombolewa Khan Tuman ni kuwa, mafanikio hayo ya kistratejia yamepatikana katika hali ambayo, tarehe 3 ya mwezi huu wa Januari, utawala wa kigaidi wa Marekani ulimuua shahidi aliyekuwa kamanda wa kikosi cha Quds cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) Luteni Jenerali Qassem Soleimani kwa tamaa kwamba, kuuliwa kwake shahidi kutazima mafanikio ya mhimili wa Muqawama katika kupambana na ugaidi. Ushindi huu muhimu umethibitisha kuwa, kuuawa shahidi Kamanda Qassem Soleimani, kunaweza kuimarisha na kuifanya thabiti zaidi azma ya wanamuqawama ya kuendeleza ushindi wa kijeshi katika mapambano yao.../