Utawala wa Kizayuni wajiepusha kuingia tena vitani na wanamuqawama wa Palestina
Waziri wa Vita wa utawala wa Kizayuni amesema kuwa utawala huo umeamua kujiepusha na kujiingiza vitani kwa mara nyingine tena na wanamuqawama wa Palestina.
Naftali Bennett amesema kuwa utawala huo hauna lengo la kuwaingiza tena wanajeshi wake katika mapigano ya siku 51 mtawalia na wanamuqawama wa Palestina.
Wanamuqawama wa Palestina katika vita vya siku 51 mwaka 2014 huko Ghaza waliwalazimisha maghasibu wa Kizayuni kufikia mapatano ya kusimamisha vita baada ya kuvurumisha makombora katika maeneo mbalimbali ya Israel; kiasi kwamba jeshi la utawala wa Kizayuni baada ya kumalizika vita hivyo mara kadhaa wa kadhaa limekiri juu ya uwezo mkubwa wa makundi ya muqawama ya Palestina.
Waziri wa Vita wa utawala wa Kizayuni aidha ameongeza kuwa utawala huo umedhamiria kwa dhati kuepuka kuingia katika vita vya tatu kati yake na Lebanon.
utawala wa Kizayuni ulipata kipigo kikali katika vita vya siku 33 mwezi Julai mwaka 2006 kati ya jeshi la utawala huo na wanamuqwama wa Harakati ya Hizbullah ya Lebanon na kulazimika kurudi nyuma kufuatia hasara na maafa makubwa waliyopata katika vita hivyo.