Kujiuzulu Tawfiq Allawi; sababu na athari zake
Muhammad Tawfiq Allawi, waziri mkuu mteule wa Iraq aliyekuwa amepewa jukumu la kuunda serikali mpya, siku ya Jumapili, ikiwa imesalia siku moja tu kabla ya kumalizika muhula huo wa kisheria aliopewa kutekeleza jukumu hilo, alikabidhi barua yake ya kujiuzulu kwa Rais Barham Salih wa nchi hiyo.
Kuanzia tarehe mosi Oktoba 2019 Iraq iligeuka uwanja wa maandamano ya kupinga serikali. Maandamano hayo, ambayo chanzo chake kilikuwa ni kulalamikia hali ya maisha na ya kijamii, yaligeuka kuwa machafuko na mapigano ya mitaani kutokana na uingiliaji wa maajinabi na usaliti uliofanywa na makundi potofu na yenye inadi, ya ndani ya nchi hiyo. Kutokana na kushadidi machafuko hayo ya mitaani, Waziri Mkuu wa wakati huo Adil Abdul-Mahdi alijiuzulu wadhifa wake, na tangu Desemba mosi hadi sasa amekuwa akiongoza kama waziri mkuu wa serikali ya mshikizo ya nchi hiyo. Baada ya mchanganyiko wa shwari na hamkani nyingi za kutangazwa majina ya watu kadhaa waliopendekezwa kushika wadhifa wa uwaziri mkuu, hatimaye mnamo tarehe mosi Februari mwaka huu, Rais Barham Salih alimteua Muhammad Tawfiq Allawi kuwa waziri mkuu mpya na kumkabidhi jukumu la kuunda serikali mpya ya nchi hiyo. Ndani ya muda wa mwezi mmoja aliopewa kuunda serikali, Allawi hakufanikiwa kutekeleza jukumu hilo na hivyo akaamua kukabidhi barua yake ya kujiuzulu kwa Rais Barham Salih.
Suali muhimu linaloulizwa ni, sababu gani zimemfanya Tawfiq Allawi ashindwe kuunda serikali mpya?
Matukio ya Iraq, hasa katika wiki hii moja ya karibuni yameonyesha kuwa kwa upande mmoja, baada ya kupita karne nzima tangu ijipatie uhuru, nchi hiyo ingali inateswa na urithi mbaya ilioachiwa wa tangu enzi za ukoloni; na kwa upande mwingine, licha ya kugubikwa na wimbi la machafuko na mvurugiko wa usalama kwa muda wa miezi mitano, makundi ya kisiasa ya Iraq yangali yanafadhilisha manufaa yao ya kimatapo na kimirengo badala ya maslahi mapana ya kitaifa; na kimsingi ni kwamba, utambulisho wa utaifa nchini Iraq umepikuliwa na kuzidiwa na ule wa matapo ya watu.
Muundo wa kidemografia, yaani idadi ya watu na ule wa kisiasa wa Iraq ni matokeo ya siasa za ukoloni wa Uingereza. Makundi ya Wakurdi, Mashia na Masuni, yameunganishwa pamoja na jiografia ya Iraq moja licha ya mikwaruzano na tofauti nyingi zilizopo baina yao; na katika kipindi chote hiki cha karne moja iliyopita, kila mara kumekuwepo na migongano na misuguano katika uhusiano wao, pamoja na mizozano na mivutano juu ya suala la madaraka. Hali hiyo inashuhudiwa hivi sasa pia ndani ya Iraq, ambapo makundi mbali mbali yamemshinikiza vikali Tawfiq Allawi kwa ajili ya kujipatia nyadhifa nyingi au muhimu zaidi za wizara katika serikali mpya aliyokusudia kuunda; na kimsingi hayakuzingatia nukta muhimu zaidi na ya msingi, ya kuipigia kura ya kuwa na imani nayo, serikali aliyopendekeza kuunda. Ukweli ni kuwa, pasi na kutilia maanani hali tete na hasasi iliyonayo nchi hiyo hivi sasa, makundi ya kisiasa ya Iraq yamepuuza maslahi mapana ya kitaifa. Katika barua yake ya kujiuzulu aliyomwandikia Rais Barham Salih, Muhammad Tawfiq Allawi, aliliashiria hilo kwa kusema, mashinikizo ya baadhi ya vyama dhidi yake, ya kufanikisha manufaa ya kichama na ya watu binafsi na si ya kitaifa, ndiyo yaliyomfanya aamue kujiuzulu.
Kutokana na hali hiyo, suali jengine muhimu la kujiuliza ni, kushindikana kuundwa serikali mpya ya Iraq kutakuwa na athari na matokeo gani?
Moja ya athari muhimu zaidi za kujiuzulu Tawfiq Allawi ni kwamba, kipindi cha serikali ya mshikizo kimemalizika, na kwa mara ya kwanza Rais wa Iraq atalazimika kushika kwa wakati mmoja wadhifa wake huo pamoja na wa uwaziri mkuu. Nukta nyingine ni kwamba, Rais atapaswa kumpendekeza waziri mkuu mwingine mpya ndani ya muda wa siku 15.
Sayyid Reza Gharabi, mtaalamu wa masuala ya Iraq anaeleza kuhusu nukta hiyo kwamba: "Hivi sasa rais atashikilia kwa muda mamlaka ya waziri mkuu mpaka atakapompendekeza yeye mwenyewe ndani ya muda wa wiki mbili waziri mkuu, bila kuhitaji mrengo ulio mkubwa zaidi bungeni." Ni jambo gumu nchini Iraq kumpendekeza waziri mkuu mpya, ambaye atakubaliwa na wananchi wanaoandamana kupinga serikali na pia atakayeweza kupata kura ya bunge ya kuwa na imani naye.
Lakini mbali na hayo, kushindwa Tawfiq Allawi kuunda serikali mpya kunaweza kuwarejesha tena waandamanaji barabarani na vilevile kuanza tena ghasia, fujo na machafuko ya mitaani; na hii ni katika mazingira ambayo, kinyume na ilivyokuwa katika miezi ya huko ya nyuma, hivi sasa Iraq inakabiliwa pia na maambukizi ya kirusi cha corona.../