Hamas: Tutakubali kubadilishana wafungwa na Israel kwa masharti
(last modified Thu, 09 Apr 2020 08:21:26 GMT )
Apr 09, 2020 08:21 UTC
  • Hamas: Tutakubali kubadilishana wafungwa na Israel kwa masharti

Mkuu wa Ofisi ya Kisiasa ya Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (Hamas) amesema harakati hiyo imeazimia kuhakikisha kuwa wafungwa wa Kipalestina walioko katika jela za Israel wanaachiwa huru katika mpango wa kubadilishana wafungwa na utawala huo wa Kizayuni.

Ismail Haniya alisema hayo jana Jumatano katika mazungumzo yake ya simu na Mikhail Bogdanov, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia na kusisitiza kuwa, mpango huo wa kubadilishana wafungwa utafanyika tu iwapo utawala pandikizi wa Israel utakubali masharti ya harakati hiyo ya muqawama.

Hata hivyo Mkuu wa Ofisi ya Kisiasa ya Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina hajatoa maelezo juu ya masharti ya Hamas ya kukubali mpango huo wa kubadilishana wafungwa na utawala pandikizi wa Israel.

Kauli ya Haniya imekuja siku moja baada ya Ofisi ya Waziri Mkuu wa utawala haramu wa Israel, Benjamin Netanyahu kusema kuwa, utawala huo uko tayari kufanya mazungumzo yasiyo ya moja kwa moja na Hamas kuhusu suala la kubadilishana wafungwa. 

Hii ni katika hali ambayo, Jumuiya ya Nchi za Kiarabu imetahadharisha kuhusu hatari kubwa inayotishia uhai wa wafungwa karibu elfu tano wa Kipalestina wanaoshikiliwa katika korokoro na jela za utawala haramu wa Israel kutokana na maambukizi ya virusi vya corona.

Wafungwa wa Kipalestina katika moja ya magereza ya Israel

Kwa mujibu wa Shakir Ammarah, mwanachama mwandamizi wa Hamas, mateka Wapalestina wanaoshikiliwa kwenye magereza ya utawala wa Kizayuni wa Israel wako kwenye mazingira mabaya na ya kutisha yaliyoachanganyika na hofu ya maambukizo ya corona na akaongeza kwamba, utawala huo haujachukua hatua yoyote kuhusiana na suala hilo huku ukiendelea kupuuza miito ya kimataifa ya kuutaka uwaachie huru mateka hao.

Mwezi uliopita, Hamas iliziomba taasisi za kisheria za kimataifa zichukue hatua za kuwanusuru mateka wa Kipalestina katika jela za utawala wa Kizayuni wa Israel kutokana na kukithiri maambukizo ya virusi vya corona katika jela hizo.

 

Tags