Answarullah ya Yemen: Malengo ya Marekani ya kumuua Qassem Soleiman hayajafikiwa
Mjumbe wa Ofisi ya Kisiasa ya Harakati ya Wananchi ya Answarullah nchini Yemen amesisitiza kuwa, Marekani haijaweza kufikia malengo yake ya kumuua shahidi Luteni Jenerali Qassem Soleimani, Kamanda wa zamani wa Kikosi cha Quds cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC).
Mohammed Al Bukhaiti ameyasema hayo katika mahojiano na kanali ya televisheni ya Al-Mayadin na kuongeza kuwa, hatua ya askari vamizi wa Marekani kumuua kigaidi Luteni Jenerali Qassem Soleimani na Abu Mahdi al-Muhandis, Naibu Mkuu wa Hashdu sh-Sha'abi ya Iraq, imeuweka hatarini uwepo wa askari hao wa Marekani nchini Iraq. Amezidi kubainisha kwamba nchini Syria na Yemen pia majeshi ya muqawama yamezidi kusonga mbele zaidi na kwamba hata kama muqawama umepoteza viongozi hao wawili, lakini Marekani haijaweza kufikia malengo yake machafu kwa kuwaua viongozi hao wa kimuqawama.
Mohammed Al Bukhaiti amesema kwamba mrengo wa muqawama umesimama kwa msingi wa matukufu ya umma wa Kiislamu na kwamba shambulio lolote dhidi ya viongozi wa mrengo huo au kutangaza vita dhidi yake, kutaufanya muqawama kuwa imara zaidi. Itakumbukwa kuwa shahidi Qassem Soleimani na Abu Mahdi al-Muhandis wakiwa pamoja na shakhsia wengine wanane walioandamana nao waliuawa shahidi tarehe tatu Januari mwaka huu, katika shambulizi la kigaidi lililotekelezwa na askari magaidi wa Marekani karibu na uwanja wa ndege wa kimataifa wa Baghdad, Iraq.