Amnesty International: Saudia imevunja rekodi ya kuwanyonga watu
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i60508-amnesty_international_saudia_imevunja_rekodi_ya_kuwanyonga_watu
Shirika la kutetea haki za binadamu Amnesty International limesema utawala wa Aal-Saud mwaka jana ulivunja rekodi ya kutekeleza hukumu ya kuwanyonga watu ndani ya mwaka mmoja nchini Saudi Arabia.
(last modified 2026-03-17T04:36:21+00:00 )
Apr 21, 2020 03:22 UTC
  • Amnesty International: Saudia imevunja rekodi ya kuwanyonga watu

Shirika la kutetea haki za binadamu Amnesty International limesema utawala wa Aal-Saud mwaka jana ulivunja rekodi ya kutekeleza hukumu ya kuwanyonga watu ndani ya mwaka mmoja nchini Saudi Arabia.

Katika ripoti yake mpya, Amnesty imesema mwaka jana 2019 utawala wa Riyadh uliwanyonga watu 184 wakiwemo wanawake sita, ambapo karibu nusu yao ni raia wa kigeni. 

Shirika hilo la kutetea haki za binadamu limesema halijawahi kurekodi idadi kubwa ya watu kunyongwa nchini Saudia kama mwaka jana, na kwamba idadi ya walionyongwa nchini humo mwaka juzi 2018 ilikuwa 149.

Clare Algar, Mkurugenzi wa Utafiti wa shirika hilo amesema kiwango cha watu kuhukumiwa kifo nchini Saudi Arabia kinatia wasiwasi mkubwa na kwamba Riyadh inatumia hukumu hizo kukandamiza wapinzani na wakosoaji wake, kwa kisingizio cha kupambana na ugaidi na kuimarisha usalama wa taifa.

Aghalabu ya watu wanaonyongwa kwa kukatwa kichwa Saudia ni raia wa kigeni

Aprili mwaka jana, watawala wa Aal-Saud licha ya upinzani mkali wa jamii ya kimataifa, waliwanyonga kwa kuwakata vichwa watu 37, aghalabu yao wakiwa Waislamu wa madhehebu ya Shia na kisha kuanika mwili wa mmoja wa Waislamu hao waliowafanyia ukatili huo kwenye kigingi hadharani kwa ajili ya kutazamwa na umati. Shirika hilo linasisitiza kuwa utawala huo wa kifalme hauheshimu thamani ya utu kwa hukumu zake hizo kikatili.

Kwa mujibu wa Amnesty International, watu 657 walinyongwa mwaka jana katika nchi mbali mbali duniani, ikilinganishwa na 690 mwaka juzi 2018.