Uturuki haina nia ya kweli katika kutetea matukufu ya Palestina
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i60618-uturuki_haina_nia_ya_kweli_katika_kutetea_matukufu_ya_palestina
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Uturuki ameukosoa utawala ghasibu wa Israel kwa kufanya njama za kunyakua na kuyaunganisha maeneo ya Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Apr 26, 2020 07:46 UTC
  • Uturuki haina nia ya kweli katika kutetea matukufu ya Palestina

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Uturuki ameukosoa utawala ghasibu wa Israel kwa kufanya njama za kunyakua na kuyaunganisha maeneo ya Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan.

Ijumaa iliyopita Hami Aksoy, sambamba na kutoa taarifa iliyoashiria makubaliano ya hivi karibuni kati ya Benjamin Netanyahu, Waziri Mkuu wa Utawala Haramu wa Kizayuni na Benny Gantz, Mkuu wa Muungano wa Blu na Nyeupe, ambayo kwa mujibu wake maeneo ya Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan yataunganishwa na maeneo mengine yanayokaliwa kwa mabavu na utawala wa Kizayuni, alisema kuwa hatua hiyo ni dhihirisho la fikra hatari ambayo inalenga kuzidhibiti ardhi za Palestina. Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Uturuki ameongeza kuwa, hatua hiyo hatari ya utawala wa Kizayuni, inaweza kuvuruga sheria za kimataifa na kuathiri msingi wa kuishi pamoja kwa amani wanadamu. Hami Aksoy aliongeza kuwa, Uturuki inaitaka jamii ya kimataifa sambamba na kupinga hatua zilizo kinyume cha sheria na za upande mmoja za utawala wa Kizayuni, kufanya juhudi za kuundwa taifa huru la Palestina mji mkuu wake ukiwa ni Baitul-Muqaddas. Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Uturuki pia alisisitiza kuwa serikali ya Ankara bado ipo pamoja na taifa la Palestina kama ambavyo inaunga mkono matukufu ya Wapalestina kwa uwezo wake wote.

Hami Aksoy, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Uturuki

Matamshi hayo ya Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Uturuki yanayobainisha kwamba irada ya Uturuki imesimama kwenye msingi wa kupigania matukufu ya wananchi wa Palestina, kidhahiri yana lengo la kupotosha fikra za waliowengi katika ulimwengu wa Kiislamu kuhusu ushirikiano mkubwa uliopo kati ya Uturuki na utawala haramu wa Israel. Inafaa kuashiria hapa kwamba Uturuki ni mmoja wa washirika wakuu wa kibiashara na kiuchumi na utawala wa Kizayuni, na daima imekuwa ikilinda uhusiano na utawala huo. Katika uwanja huo, Hatice Karahan, Mshauri wa Ngazi ya juu wa Kiuchumi wa Rais Recep Tayyip Erdoğan ameutaja uhusiano wa kiuchumi wa Uturuki na Israel katika mahojiano na Shirika la Habari la Deutsche Welle kuwa ni wa 'mlingano' na wenye faida kwa pande mbili. Aidha Bi Hatice Karahan amesema kuwa Uturuki inauuzia utawala wa Kizayuni vifaa vya magari, vyuma, aluminiamu na vifaa vya umeme,  na kununua kutoka kwa utawala huo nishati na mafuta. Itakumbukwa kuwa Uturuki iliutambua rasmi utawala wa Kizayuni mwaka 1948. Suala hilo ni mfano halisi wa kuyafanyia hiyana mapambano ya Wapalestina, na katika miongo yote iliyopita, licha ya kuwepo matamshi yake ya eti kuwaunga mkono Wapalestina, lakini bado haijawahi kubadili msimamo kuhusu uhusiano wake na utawala huo ghasibu. Kuhusiana na suala hilo Christian Berkel, mkuu wa taasisi ya Heinrich Böll ya nchini Uturuki anasema kuwa, serikali ya Ankara inaendelea kulinda uhusiano wake na utawala wa Kizayuni kwa sababu za kiusalama na kiuchumi.

Madai ya Uturuki ya kuitetea Palestina ni hadaa tupu, kwani ina uhusiano mkubwa na Israel

Hii ni katika hali ambayo uchunguzi wa maoni wa kila mwaka uliofanywa na Chuo Kikuu cha 'Kadir Has' cha mjini Istanbul kuhusiana na suala hilo umezungumzia 'siasa za kigeni za Uturuki mwaka 2019' kwamba asilimia 81.3 ya raia wa Uturuki wanaiona Marekani kuwa ni hatari kwa nchi hiyo, huku asilimia 70.8 wakiuona utawala haramu wa Kizayuni kuwa ndio tishio kwa usalama wa nchi hiyo. Kwa ajili hiyo tunaweza kusema kuwa, Rais Recep Tayyip Erdoğan hazingatii mitazamo ya ndani ya nchi yake katika uga wa mahusiano ya Uturuki na utawala wa Kizayuni, kama ambavyo hapatwi na hofu juu ya hatari inayoyakabili matukufu ya Palestina na ulimwengu wa Kiislamu. Maelezo ya Wizara ya Mambo ya Nje ya Uturuki ni matamshi matupu ambayo Uturuki inakusudia kuyatumia kuvutia uungaji mkono wa ulimwengu wa Kiislamu na kwa upande mwingine yamsaidie Erdoğan katika midahalo ya ndani nchini. Ukweli ni kwamba lau kama matamshi ya Uturuki yangekuwa ni ya kweli katika kusimama imara mkabala wa utawala wa Kizayuni na kuunga mkono matukufu ya watu wa Palestina, basi ingetakiwa katika hatua ya kwanza ikate uhusiano wa kiuchumi na kiusalama na utawala huo bandia wa Kizayuni.