HAMAS yatahadharisha kuhusu njama za kuiyahudisha Palestina
(last modified Thu, 07 May 2020 07:53:10 GMT )
May 07, 2020 07:53 UTC
  • HAMAS yatahadharisha kuhusu njama za kuiyahudisha Palestina

Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS imeutaja mpango wa kuunganisha Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan na ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu (Israel) kama njama hatari zaidi ya kuziyahudisha ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu.

Abdul Latif al-Qanoo, msemaji wa HAMAS alisema hayo jana Jumatano na kufafanua kuwa, "kwa mujibu wa mpango huo, asilimia 38 ya Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan itaunganishwa na ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu (Israel) na kuvipa 'uhalali' kwa asilimia 70 vitongoji vya walowezi wa Kizayuni katika eneo hilo."

Ameeleza bayana kuwa, ili kuweza kukabiliana na njama hizi mpya za Wazayuni maghasibu, kunahitajika harakati mpya za utaifa nchini Palestina sambamba na Mamlaka ya Ndani ya Palestina kuunga mkono mhimili wa muqawama.

Ujenzi wa vitongoji vya walowezi wa Kizayuni huko Palestina inayokaliwa kwa mabavu na Israel

Wiki iliyopita pia, Saeb Erekat, Mkuu wa Kamati ya Utendaji ya Harakati ya Ukombozi wa Palestina (PLO) alisema Mamlaka ya Ndani ya Palestina imetuma ujumbe kwa nchi kadhaa duniani, na kuwasisitizia kuhusu udharura wa kuwepo kikao cha kimataifa kwa lengo la kuhitimisha ukaliwaji mabavu wa ardhi za Palestina, kuanzishwa dola la Palestina mji mkuu wake ukiwa ni Quds Tukufu (Jerusalem) na kutatuliwa masuala mengine hasa kadhia ya wakimbizi na mateka wa Palestina.

Benjamin Netanyahu, Waziri Mkuu wa utawala wa Kizayuni wa Israel na Benny Gantz, Spika wa bunge la utawala wa Kizayuni (Knesset) ambaye anashirikiana na Neytanyahu katika serikali ya mseto hivi karibuni walitangaza kuwa, kuanzia mwezi Julai, sehemu ya Ukingo wa Magharibi itaunganishwa na ardhi zinazokaliwa kwa mabavu.

Tags