Haniyah: Kuufanya wa kawaida uhusiano na Israel ni kosa lisilosameheka
(last modified Sat, 09 May 2020 12:33:27 GMT )
May 09, 2020 12:33 UTC
  • Haniyah: Kuufanya wa kawaida uhusiano na Israel ni kosa lisilosameheka

Mkuu wa Ofisi ya Kisiasa ya Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS amesema njama zozote zinazolenga kuufanya wa kawaida uhusiano baina ya mataifa ya Kiarabu na utawala haramu wa Israel ni kosa ambalo halina msahama.

Ismail Haniyah amezikosoa baadhi ya nchi za Kiarabu zinazofanya jitihada za kuhakikisha kuwa zinakuwa na uhusiano wa kawaida na utawala wa Kizayuni na kueleza bayana kuwa, kitendo hicho ni sawa na kulipiga kisu cha mgongoni taifa la Palestina.

Amebainisha kuwa, "wale ambao wanashiriki katika jitihada za kuufanya wa kawaida uhusiano na adui Mzayuni wanaushajiisha utawala huo haramu uendelee kuwafanyia Wapalestina vitendo vya kigaidi."

Afisa huyo wa ngazi za juu wa harakati ya muqawama ya HAMAS ya Palestina ametoa mwito wa kuchukuliwa hatua za kivitendo za kuifanya kosa la jinai mipango yoyote ya kutaka kuwa wa kawaida uhusiano baina na Israel na Waarabu.

Harakati za Muqawama wa Kiislamu za Palestina HAMAS na Jihadul-Islami

Hapo jana, Harakati za Muqawama wa Kiislamu za Palestina HAMAS na Jihadul-Islami zilikosoa vikali mpango wa baadhi ya nchi za Kiarabu wa kutaka kurejea kwenye meza ya mazungumzo na utawala haramu wa Israel na kusisitiza kuwa, kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala huo bandia katu haikubaliki kwani ni kwenda kinyume kabisa na maslahi ya wananchi wa Palestina.

Haya yanajiri wakati huu ambapo televisheni ya MBC ambayo inamilikiwa na Saudi Arabia inarusha hewani katika mwezi huu wa Ramadhani filamu za mfululizo za "Makhraj 7" na "Ummu Harun" kwa lengo la kuisafisha sura ya utawala wa Kizayuni na kuufanya uonekane kuwa ni utawala wenye utu na ubinadamu.

Tags