Hamas yalaani mashambulizi ya Israel nchini Syria
Msemaji wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (Hamas) amelaani mashambulizi ya makombora ya utawala wa Kizayuni wa Israel katika ardhi ya Syria.
Hazim Qassim amelaani mashambulizi ya jana usiku ya utawala wa Kizayuni huko Syria na kuzitaja Marekani na nchi za Kiarabu kuwa ndizo zinazoutia kiburi utawala huo kuzishambulia nchi nyingine za eneo hili.
Msemaji wa Hamas ameongeza kuwa, Maghasibu wa Kizayuni wanazishambulia nchi za Kiislamu kwa uungaji mkono wa Marekani huku nchi za Kiarabu zikifanya juhudi za kuhuisha uhusiano wao na Wazayuni.
Mfumo wa ulinzi wa anga wa jeshi la Syria jana usiku uliingilia kati na kuzuia makombora yaliyorushwa na ndege za kivita za Israel kuelekea katika kitongoji cha mji wa Hama.
Shirika la habari la Syria (SANA) limeripoti kuwa, kambi ya jeshi la anga ya Masyaf ndiyo iliyokuwa imekusudiwa na utawala wa Kizayuni katika mashambulizi hayo, hata hivyo yalizuiwa na kusambaratishwa na mfumo imara wa ulinzi wa anga wa jeshi la Syria.