Bahrain; hukumu mbili za kifo katika siku moja
Mahakama ya juu ya Bahrain tarehe 15 Julai ilitoa hukumu ya kunyongwa vijana wawili wa nchi hiyo kwa kutegemea ushahidi bandia
Malalamiko na maandamano ya wananchi wa Bahrain dhidi ya utawala dhalimu wa nchi hiyo yalianza tarehe 14 Februri mwaka 2011. Mwanzoni walikuwa wakitaka kufanyika mabadiliko katika mfumo wa utawala wa nchi hiyo hasa kuondolewa ubaguzi, lakini taratibu maandamano hayo yalichukua sura mpya ya ghasia kufuatia hatua ya utawala wa Saudia ya kutuma askari wake katika nchi hiyo jirani kwa ajili ya kuwakandamiza wapinzani wa utawala wa Aal Khalifa. Utawala huo umekuwa ukitumia mbinu tofauti za kidikteta na za mkono wa chuma dhidi ya wapinzani ikiwa ni pamoja na kutolewa hukumu za kifo dhidi yao.
Tokea mwaka 2011 hadi sasa utawala wa Aal Khalifa umetoa hukumu bandia 40 za kifo dhidi ya watu wanaolalamikia uongozi mbovu wa watawala ambao ni vibaraka wa Saudia na nchi za Magharibi. Mahakama ya Juu ya Bahrain imekuwa ikiwaelekezea wapinzani wa utawala huo tuhuma bandia kama vile kushambulia askari usalama au kupanga njama za kutekeleza operesheni za kigaidi na hatimaye kuwapa vifungo vya muda mrefu na kutoa hukumu za kifo dhidi yao. Hukumu mbili zilizotolewa hivi karibuni dhidi ya vijana wawili wa nchi hiyo kwa kwa madai bandia kuwa waliwashambulia askari usalama pia zimetolewa kwa msingi huo huo. Hii ni katika hali ambayo vijana hao hawakuwa na kosa jingine ghairi ya kuukosoa utawala wa Manama kwa kuwakandamiza raia na kutozingatia matakwa yao.
Nukta nyingine ni kwamba utawala huo unawatesa wapinzani wake wa kisiasa na kuwalazimisha kukiri makosa wasiyohusika nayo kwa kutegemea tuhuma zisizo na msingi wowote. Mashirika ya kutetea haki za binadamu ya Human Rights Watch na Kituo cha Haki za Binadamu na Demokrasia cha Bahrain yalitangaza siku chache zilizopita kwamba watu waliohukumiwa kifo wanasisitiza kwamba waliteswa na askari usalama na kulazimishwa kukiri makosa ambayo hawakuyafanya.
Tunaweza kusema kuwa uadilifu ambao unapaswa kuwa muhimili muhimu zaidi katika chombo na mfumo wa mahakama ya nchi yoyote ile, ni jambo lisiloonekana kabisa katika mahakama za Bahrain. Tuhuma bandia, kutolewa hukumu za kidhalimu na hasa kunyongowa na watuhumiwa kuteswa na kulazimishwa kukiri makosa wasiyohusika nayo ni vielelezo vya wazi vinavyoashiria kwamba mfumo wa mahakama wa Bahrain sio huru na wala hauwezi kutegemewa katika kutoa hukumu za kiuadilifu.
Kuhusu suala hilo, Jamal Firouz, mbunge wa zamani wa Bahrain ambaye pia ni mkuu wa Taasisi ya Demokrasia na Haki za Binadamu ya Bahrain siku chache zilizopita alikosoa mfumo wa mahakama wa nchi hiyo pamoja na hukumu zake za kidhalimu zikiwemo zile zinazotolewa dhidi ya wanaharakati wa kisiasa na kusema, mahakama zimekuwa za kisiasa, zisizo huru na ambazo zinatumiwa na watawala kwa ajili ya maslahi yao binafsi.
Kutolewa kiholela hukumu za kifo dhidi ya raia wa Bahrain kabla ya jambo lolote lile kunathibitisha kwamba utawala wa Manama umekosa uhalali wa kutawala nchi na ndio maana ukawa unatumia nguvu, mateso na mabavu kupitia mahakama dhidi ya wapinzani wake wa kisiasa na wananchi wa kawaida wanaopigania haki zao za msingi. Nukta nyingine ni kuwa utawala wa Bahrain umetoa hukumu hizo za kidhalimu dhidi ya raia wa nchi hiyo katika kipindi ambacho eneo zima la Asia Magharibi limeshughulishwa na masuala mengine muhimu zaidi. Hivi sasa eneo hili, kama yalivyo maeneo mengine ya dunia, kwa upande mmoja limeshughulishwa na janga la kuenea virusi hatari vya corona na katika upande wa pili linatatizwa na makabiliano ya makundi ya mapambano ya Palestina na utawala haramu wa Israel unaopanga njama za kuziunganisha ardhi za Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan na maeneo mengine unayoyakalia kwa mabavu kufikia tarehe mosi mwezi ujao.
Nukta ya mwisho ni kwamba licha ya kuwa hukumu za kifo zilizotolewa na utawala wa Bahrain dhidi ya raia wa nchi hiyo ni za kisiasa, lakini jambo la kusikitisha ni kuwa jamii ya kimataifa na hasa Umoja wa Mataifa imekaa kimya na kutochukua hatua yoyote ya kukabiliana au kupinga hukumu hizo za kidhulma. Kimya cha madola ya Magharibi na Umoja wa Mataifa, ambayo ni ishara ya kuunga mkono vitendo vya utawala wa Aal Khalifa, ni sababu kuu ya utawala huo kuendelea kumea pembe na kutoa hukumu za kidhulma na kisiasa dhidi ya wanaharakati wa kisiasa kupitia tuhuma bandia na zisizo na msingi.