Rais wa China: Kadhia ya Palestina ndiyo kuu zaidi Asia Magharibi
Rais Xi jingping wa China amesema kadhia ya Palestina ndilo swala kuu zaidi hivi sasa katika eneo la Asia Magharibi.
Rais wa China amesema hayo katika mazungumzo yake ya simu na Mahmoud Abbas, Rais wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina na kuongeza kuwa: Msimamo wa China kwa kadhia ya Palestina ni wa kudumu na ulio wazi. Tunaunga mkono matakwa halali ya Wapalestina na jitihada zote zinazofanyika za kuipatia ufumbuzi kadhia ya Palestina.
Huku akiitaka jamii ya kimataifa iwe na msimamo wa kiadilifu kwa kadhia ya Palestina, Rais Xi jingping wa China ameeleza bayana kuwa, Beijing ina azma ya kuendelea kutekeleza wajibu wake wa kuhakikisha kuwa suala la Palestina linapatiwa ufumbuzi wa kudumu na usioegemea upande mmoja haraka iwezekanavyo.
Katika sehemu nyingine ya mazungumzo yake na Rais wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina, Rais wa China ameeleza bayana kuwa, nchi yake itandelea kuwasaidia wananchi na serikali ya Palestina katika mapabano dhidi ya janga la corona huku akisisitiza kuwa, China na Palestina zina uhusiano wa dhati uliojengeka katika misingi ya maslahi ya pamoja.
Kwa upande wake, Mahmoud Abbas, Rais wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina mbali na kuishukuru China kwa misaada yake kwa Wapalestina kwa ajili ya kukabiliana na ugonjwa wa Covid-19, amebainisha kuwa China imedhihirisha kuwa ni katika marafiki wa kweli na wa kuaminika wa Palestina.
Kadhalika ameishukuru serikali ya Beijing kwa jitihada zake za kupigania haki halali na maslahi ya wananchi madhulumu wa Palestina.