HAMAS yaonya kuhusu njama ya kuuyahudisha Msikiti wa Ibrahim (as)
Msemaji wa Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Palestina HAMAS ametoa onyo dhidi ya hatua unazopanga kuchukua utawala wa Kizayuni wa Israel za kuuyahudisha Msikiti wa Nabii Ibrahim (as) ulioko katika mji wa Al Khalil huko Palestina inayokaliwa kwa mabavu.
Abdulatif al Qanoa amesema, maamuzi yaliyopangwa kutekelezwa na utawala wa Kizayuni ya kuubadilisha muundo wa Msikiti wa Ibrahim (as) ulioko katika mji wa Al-Khalil ni uvamizi na uchokozi mwengine mpya dhidi ya matukufu ya Kiislamu.
Al Qanoa amebainisha kuwa, hatua hiyo ya utawala ghasibu wa Kizayuni ni ukiukaji wa wazi wa sheria za kimataifa na akasisitiza kwamba: Miji na matukufu ya Waislamu yatabaki kuwa na utambulisho wao wa Kiarabu na Kiislamu.
Msikiti wa Ibrahim (as) uko katika kitongoji cha kale cha Al Khalil kusini mwa Ufukwe wa Magharibi wa Mto Jordan huko Palestina inayokaliwa kwa mabavu. Kwa mujibu wa baadhi ya Hadithi, ndani ya msikiti huo kuna kaburi la Nabii Ibrahim (as) na mkewe Sarah na vile vile makaburi ya Manabii Is-haq na Yaaqub (as) na ya wake zao.../