Hamas: Ghaza inakabiliwa na changamoto 3 kwa wakati mmoja
Mkuu wa Ofisi ya Kisiasa ya Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (Hamas) amesema, eneo la Ukanda wa Ghaza hivi sasa linakabiliwa na changamoto tatu kwa wakati mmoja. Amesema, hatua inapasa zichukuliwe ili kutatua changamoto hizo.
Ismail Hania ameongeza kuwa: changamoto ya kwanza ni kuzingirwa Ghaza na taathira za mzingiro kwa wakazi wa eneo hilo, changamoto ya pili ni hali ya raia walioambukizwa virusi vya corona nje ya vituo vya karantini, na changamoto ya tatu ni namna ya kukabiliana na uvamizi na chokochoko za mara kwa mara za utawala wa Kizayuni.
Hania amesema kuwa utawala wa Kizayuni ni mhusika kamili wa hali ya sasa katika Ukanda wa Ghaza na akaongeza kuwa: utawala huo inapasa uhitimishe mzngiro huo haraka iwezekanavyo sambamba na kukomesha uvamizi wake dhidi ya Wapalestina. Amesema kuwa, utawala wa Kizayuni unapaswa uruhusu kuingizwa vifaa tiba huko Ghaza kwa ajili ya kukabiliana na maambukizi ya corona.
Wakati huo huo, Harakati ya Jihad Islami ya Palestina pia imetoa taarifa ikisisitiza juu ya jitihada inazofanya ili kuvunja mzingiro huko Ghaza na kuutahadharisha utawala wa Kizayuni na kukwamisha utekelezaji wa masharti yanayohusiana na kuhitimisha mzingiro huo tajwa.
Utawala wa Kizayuni umeliwekea mzingiro wa ardhini, baharini na angani eneo la Ukanda wa Ghaza tangu mwaka 2017.