HAMAS yasisitiza kuendeleza uhusiano wa kistratejia na Hizbullah ya Lebanon
Kiongozi mwandamizi wa Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Palestina HAMAS amesema, uhusiano wa kistratejia baina ya makundi ya ukombozi na muqawama na Hizbullah ya Lebanon utapelekea kukombolewa Palestina kutoka kwenye makucha ya maghasibu wa Israel.
Osama Hamdan ameyasema hayo katika mahojiano na kanali ya televisheni ya Al Mayadeen na kusisitiza kuwa, kupinga kukaliwa kwa mabavu eneo la Ufukwe wa Magharibi na vile vile mpango wa Kimarekani na Kizayuni wa 'Muamala wa Karne' ni msimamo wa makundi yote ya Palestina.
Hamdan ameongeza kuwa, Hamas haitarudi nyuma katika msimamo wake kuhusiana na mpango wa kitaifa wa kistratejia iliopendekeza wa kutaka Palestina ikombolewe kupitia muqawama.
Kiongozi huyo mwandamizi wa Hamas ameashiria pia kikao kitakachofanyika kati ya Mkuu wa ofisi ya kisiasa ya Hamas na Katibu Mkuu wa Hizbullah ya Lebanon na akaeleza kwamba, uhusiano wa Hamas na Hizbullah ni wa kistratejia na wa tangu na tangu.
Mkuu wa ofisi ya kisiasa ya Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Palestina HAMAS, Ismail Haniya, jana jioni aliwasili mji mkuu wa Lebanon, Beirut na anatazamiwa kukutana na kufanya mazungumzo na Katibu Mkuu wa Hizbullah, Sayyid Hassan Nasrullah.
Mkuu wa ofisi ya kisiasa ya Hamas leo anatazamiwa pia kushiriki katika kikao cha makundi ya muqawama ya Palestina kitakachofanyika mjini Beirut.../