Ismail Hania: Mapambano ndio chaguo bora la kukabiliana na wavamizi
Mkuu wa Ofisi ya Kisiasa ya Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS ametangaza kuwa, muqawama na mapambano ndio njia bora na athirifu kwa ajili ya kukabiliana na utawala haramu wa Israel.
Ismail Hania amesema hayo katika mahojiano aliyofanyiwa na Kanali ya televisheni ya al-Manar ya Lebanon ambapo ameashiria hatua ya kisaliti na khiyana ya watawala wa Imarati dhidi ya taifa la Palestina na kusema kuwa, Abu Dhabi haina kisingizio chochote kile cha kuhalalisha hatua yake hiyo ya kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala huo ghasibu.
Kiongozi huyo wa Harakati ya Hamas amesema wazi kuwa, hatua hiyo ya Imarati imefanyika kwa ajili ya kutoa huduma kwa Rais Donald Trump wa Marekani na Waziri Mkuu wa utawala vamizi wa Israel Benjamin Netanyahu.
Mkuu wa Ofisi ya Kisiasa ya Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS amesisitiza kuwa, ili kukabiliana na mipango michafu ya utawala bandia wa Israel kama kupora sehemu ya ardhi ya Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan, ujenzi wa vitongoji vya walowezi wa Kiyahudi katika maeneo ya Wapalestina na mwenendo wa kuanzishwa uhusiano wa kawaida na Israel kuna haja ya kutekelezwa mkakati na stratejia ya kitaifa.
Amesema, Hamas imo mbioni kuandaa mpango wa kitaifa wenye lengo la kuimarisha muqawama wa wananchi, kuifanya Harakati ya Ukombozi wa Palestina kuwa amilifu na kuhitimisha migawanyiko na hitilafu za ndani baina ya Gaza na Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan.