Picha za watawala wa Bahrain na Imarati zachomwa moto Ghaza, Palestina
Wakazi wa Ukanda wa Ghaza huko Palestina wamechoma moto picha za watawala wa Bahrain na Umoja wa Falme za Kiarabu (Imarati) kutokana na nchi hizo mbili za Kiarabu kutangaza uhusiano wa kawaida na utawala wa Kizayuni wa Israel.
Duru za habari zimeripoti habari hiyo na kuongeza kuwa, wananchi wa Ghaza, usiku wa kuamkia leo wamekusanyika katikati ya mji wa Deir al Balah huko Ghaza na kuchoma moto picha za mfalme wa Bahrain, Hamad bin Isa Aal Khalifa ikiwa ni ishara ya kulaani hatua ya nchi hiyo ya kutangaza uhusiano wa kawaida na utwala katili wa Israel.
Vile vile wananchi hao wa Ghaza wamechoma moto pia picha za waziri mkuu wa utawala wa Kizayuni, Benjami Netayahu, rais wa Marekani, Donald Trump, Mohamad bin Zaid mrithi wa kiti cha ubalme wa Abu Dhabi na Muhammad bin Rais Aal Maktoum, rais na waziri mkuu wa Umoja wa Falme za Kiarabu (Imarati).
Katika kipindi cha chini ya mwezi mmoja tangu Imarati ilipotangaza kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala wa Kizayuni wa Israel, utawala wa kiimla na kidikteta wa Bahrain nao umefuata mkumbo huo, ambapo juzi tarehe 11 Septemba, rais wa Marekani alitangaza rasmi kuanzishwa uhusiano wa kawaida baina ya Bahrain na utawala wa Kizayuni unaoikalia kwa mabavu Palestina. Usaliti huo wa nchi hizo za Kiarabu umelalamikiwa na unaendelea kulalamikiwa vikali.
Balozi wa Palestina Khalid Aarif ameondoka katika mji mkuu wa Bahrain, Manama, ikiwa ni kulalamikia usaliti wa nchi hiyo wa kutangaza uhusiano wa kawaida na utawala dhalimu wa Israel.
Ijumaa usiku, baada ya Donald Trump kutangaza kuanzishwa uhusiano wa kawaida baina ya Bahrain na utawala wa Kizayuni, serikali ya Mamlaka ya Ndani ya Palestina ililaani vikali usaliti huo wa viongozi wa Bahrain na kusema kuwa, kitendo hicho ni sawa na kukisaliti Kibla cha Kwanza cha Waislamu na malengo matukufu ya ukombozi wa Palestina.