Jihadul Islami: Muqawama ndio utakaowafurusha Wazayuni Palestina
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i63464-jihadul_islami_muqawama_ndio_utakaowafurusha_wazayuni_palestina
Mjumbe wa ngazi za juu wa harakati ya Jihadul Islami ya Palestina amesema kuwa, muqawama ndiyo njia pekee ya kuwatimua Wazayuni katika ardhi wanazozikalia kwa mabavu.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Sep 16, 2020 21:51 UTC
  • Jihadul Islami: Muqawama ndio utakaowafurusha Wazayuni Palestina

Mjumbe wa ngazi za juu wa harakati ya Jihadul Islami ya Palestina amesema kuwa, muqawama ndiyo njia pekee ya kuwatimua Wazayuni katika ardhi wanazozikalia kwa mabavu.

Muhammad al Hindi, alisema hayo jana na kufafanua kwamba, mashambulizi ya maroketi yaliyofanywa na makundi ya muqawama wa Palestina ni majibu ya jinai za kila siku za Wazayuni dhidi ya Wapalestina na kwamba maroketi ya wanamapambano wa Palestina yatafuta ghururi na majivuno ya kupindukia ya Marekani na utawala wa Kizayuni.

Amma kuhusu hatua ya nchi bili za Kiarabu za Umoja wa Falme za Kiarabu (Imarati) na Bahrain ya kutangaza uhusiano wa kawaida na utawala wa Kizayuni wa Israel, al Hindi amesema, mapambano yajayo sasa yatafanyika katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan, sehemu ambayo utawala wa Kizayuni umeifanya kuwa ndicho kitovu cha kuendeshea njama zake dhidi ya Wapalestina.

Dk Muhammed al Hindi katika mazungumzo na waandishi wa habari

 

Kiongozi huyo mwandamizi wa Jihadul Islami ya Palestina pia amesema, makubaliano yaliyofikiwa baina ya nchi mbili za Kiarabu za Imarati na Bahrain na utawala wa Kizayuni wa Isrel ni kwa ajili ya kumtumikia rais wa Marekani tu, Donald Trump, na kwamba ni Marekani ndiyo inayozidhibiti nchi hizo zinazotia saini mapatano na Wazayuni

Baada ya kutangaza uhusiano wa kawaida na utawala pandikizi wa Kizayuni unaokikalia kwa mabavu Kibla cha Kwanza cha Waislamu, juzi Jumanne, Imarati na Bahrain zilikwenda kutia saini makubaliano hayo mbele ya Donald Trump na waziri mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, huko Washington, Marekani.