Hamas: Maghasibu watafukuzwa katika ardhi ya Palestina
Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (HAMAS) imetangaza kuwa, utawala haramu wa Israel utafukuzwa katika ardhi inayokaliwa kwa mabavu ya Palestina.
Hassan Yusuf ambaye ni mjumbe wa ngazi za juu wa Hamas amesema kuwa, harakati hiyo inafanya jitihada za kukomesha hitilafu baina ya makundi mbalimbali ya kupigania ukombozi wa Palestina na kwamba haitarudi nyuma hadi utawala haramu utakapofukuzwa katika ardhi inayokaliwa kwa mabavu.
Hassan Yusuf amesema kuwa, harakati ya Hamas imekula kiapo kwa taifa la Palestina kwamba itadumisha njia hiyo ya mapambano hadi utawala wa Kizayuni wa Israel utakapofukuzwa kikamilifu katika ardhi ya Palestina na kurejeshwa haki zote za taifa hilo.
Mjumbe huyo wa Hamas amesisitiza kuwa Wapalestina hawana njia nyingine ghairi ya kuungana na kuwa na umoja ambao ndio wenzo pekee wa kukabiliana na njama zote zinazofanywa dhidi ya Palestina.
Amesema kuwa Palestina inakabiliwa na changamoto kubwa kama mpango wa Muamala wa Karne na kupuuzwa haki zake. Hassan Yusuf amesema umoja na mshikamano wa Wapalestina ndio silaha ya kushinda changamoto hizo.