UN: Israel imebomoa zaidi ya nyumba 500 za raia wa Wapalestina
(last modified Tue, 29 Sep 2020 07:00:49 GMT )
Sep 29, 2020 07:00 UTC
  • UN: Israel imebomoa zaidi ya nyumba 500 za raia wa Wapalestina

Umoja wa Mataifa umetangaza kuwa utawala wa Kizayuni wa Israel umebomoa zaidi ya nyumba mia tano za raia wa Palestina.

Ripoti iliyotolewa jana na Ofisi ya Uratibu wa Misaada ya Kibinadamu ya Umoja wa Mataifa (OCHA) imesema kuwa, tangu mwanzoni mwa mwaka huu utawala wa Kizayuni wa Israel umebomoa nyumba 506 za Wapalestina. OCHA imesema 134 kati ya nyumba hizo zimebolewa katika Quds inayokaliwa kwa mabavu. 

Ripoti hiyo ya Umoja wa Mataifa imeongeza kuwa wiki mbili zilizopita peke yake Israel ilibomoa nyumba 22 za raia wa Palestina. Ocha imesema baadhi ya nyumba hizo zimebomolewa kwa kisingizio kwamba hazikuwa na vibali na nyingine kwa kuwekewa kodi kubwa kupita kiasi. 

Wakati huo huo Mratibu wa Masuala ya Kibinadamu wa Umoja wa Mataifa, Jamie McGoldrick amesema Israel imezidisha bomoa bomoa ya nyumba za Wapalestina katika miezi ya karibuni sambamba na maambukizi ya virusi vya corona. 

UN: Israel imebomoa mamia ya nyumba za raia wa Palestina mwaka huu wa 2020

Utawala haramu wa Israel umekuwa ukiboa nyumba na maeneo ya kihistoria ya Palestina kwa shabaha ya kubadilisha muundo na jiografia ya maeneo hayo na kuyapa sura ya kiyahudi kwa kujenga vitongoji vya walowezi wa kizayuni katika maeneo hayo. 

Itakumbukwa kuwa Disemba mwaka 2016 Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lilipasisha azimio nambari 2334 lililoutaka utawala haramu wa Israel kusitisha mara moja shughuli zote za ujenzi wa vitongoji vya walowezi wa Kiyahudi katika ardhi zinayokaliwa kwa mabavu ya Palestina.