Awamu ya pili ya ibada ya Umrah yaanza Saudia
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i63998-awamu_ya_pili_ya_ibada_ya_umrah_yaanza_saudia
Wizara ya Hija na Umrah Saudia imetangaza kuwa watu 250,000 wataruhusiwa kushiriki katika awamu ya pili ya ibada ya Umrah ikiwa ni katika mpango wa kuanza hatua kwa hatua ibada hiyo.
(last modified 2026-08-17T09:53:57+00:00 )
Oct 13, 2020 08:50 UTC
  • Awamu ya pili ya ibada ya Umrah yaanza Saudia

Wizara ya Hija na Umrah Saudia imetangaza kuwa watu 250,000 wataruhusiwa kushiriki katika awamu ya pili ya ibada ya Umrah ikiwa ni katika mpango wa kuanza hatua kwa hatua ibada hiyo.

Taarifa ya wizara hiyo imesema duru ya pili ya Umrah itaanza Oktoba 18 na duru ya tatu, ambayo itawajumuisha wageni kutoka nje ya Saudia itaanza Novemba 1.

Taarifa hiyo imesema kila nchi itapangiwa idadi maalumu ya raia wake wanaoweza kushiriki katika Umrah.

Saudia ilipiga marufuku ibada ya Umrah zaidi ya miezi sita iliyopita baada ya kuibuka janga la corona. Mwaka huu pia kutokana na corona, ni idadi ndogo sana ya Waislamu walioweza kutekeleza ibada ya Hija na wote walikuwa ni wakaazi wa Saudia.

Msikiti wa Mtume SAW  (Al-Masjid an-Nabawī) mjini Madina

Mbali na kufika katika Msikiti Mtakatifu wa Makkah, wanaoenda Umrah pia wataruhusiwa kutembelea Al Rawdah Al Sharifa na eneo la zamani la Msikiti wa Mtume (SAW) mjini Madina.

Utawala wa Saudia umekuwa ukikosolewa kwa kutozihusisha nchi za Kiislamu duniani katika maamuzi yake kuhusu ibada za Hija na Umrah. Hatua ya Saudia ya kujichukulia maamuzi ya upande mmoja pia imekosolewa na maulamaa wa Kiislamu duniani.