Maelfu waandamana tena kumshinikiza Benjamin Netanyahu ajiuzulu
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i64088-maelfu_waandamana_tena_kumshinikiza_benjamin_netanyahu_ajiuzulu
Maelfu ya wakazi wa Palestina inayokaliwa kwa mabavu (Israel) usiku wa kuamkia leo wamefanya maandamano makubwa huko Quds na miji mingine inayokaliwa kwa mabavu wakitaka kujiuzulu Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu.
(last modified 2026-08-14T10:24:44+00:00 )
Oct 18, 2020 04:49 UTC
  • Maelfu waandamana tena kumshinikiza Benjamin Netanyahu ajiuzulu

Maelfu ya wakazi wa Palestina inayokaliwa kwa mabavu (Israel) usiku wa kuamkia leo wamefanya maandamano makubwa huko Quds na miji mingine inayokaliwa kwa mabavu wakitaka kujiuzulu Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu.

Waandamanaji hao wenye hasira wakiwa wamebeba mabango na maberamu walisika wakipiga nara dhidi ya Benjamin Netanyahu na kumtaka ajiuzulu wadhifa wake huo na kujitenga kabisa na siasa kutokana kukabiliwa na kashfa nyingi za ufisadi.

Aidha waandamanaji hao wanasema kuwa, Benjamin Netanyahu na serikali yake wameshindwa kuzipatia ufumbuzi changamoto zinazowakabili kama janga la corona na kuvurugika uchumi katika jamii ya Israel.

Waandamanaji hao wamejitokeza kwa wingi kushiriki na kupuuza sheria kali iliyopasishwa hivi karibuni kwa ajili ya eti kudhibiti wimbi jipya la maambukizi ya virusi vya corona.

Benjamin Netanyahu, Waziri Mkuu wa utawala haramu wa Israel ambaye yuko katika mashinikizo makali yanayomtaka ajizulu

 

Maandamano hayo yamefanyika siku chache tu baada ya Bunge la utawala huo haramu kupasisha sheria inayokataza watu kuandamana zaidi ya kilomita moja kutoka katika majumba yao.

Katika miezi ya hivi karibuni Israel imekuwa ikishuhudia maandamano makubwa ambayo yanamtaka Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu ajiuzulu kutokana na kile wanachosema waandamanaji kwamba, ni kushindwa kwake kukabiliana na changamoto zinazowakabili.

Maandamano hayo yanafanyika kila Jumapili na kuhudhuriwa na maelfu ya watu. Netanyahu na baraza lake la mawaziri wanalaumiwa kwamba, badala ya kutanguliza mbele matatizo ya kiafya na kiuchumi yanayoisumbua Israel kwa sasa, wameng’ang’ania kusukuma mbele gurudumu la mipango ya kuzikalia kwa mabavu ardhi za Palestina.