Kashani: Uchaguzi wa Bunge utabatilisha njama za adui
Hatibu wa Swala ya Ijumaa iliyoswaliwa leo hapa mjini Tehran amesema kuwa chaguzi zitakazofanyika Februari 26 hapa nchini zinatoa jibu kali kwa njama zinazofanywa na maadui wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
Ayatullah Muhammad Emami Kashani ametilia mkazo nafasi muhimu ya uchaguzi wa Februari 26 hapa nchini katika kuimarisha utawala wa Kiislamu hapa nchini na kusema: Mshikamano wa kitaifa hususan mahudhurio makubwa ya wananchi katika masanduku ya kupigia kura yanaweza kubatilisha harakati za madola ya kibeberu dhidi ya uchaguzi wa Bunge na ule wa Baraza la Wataalamu Wanaomchagua Kiongozi Mkuu wa Iran.
Hatibu wa Swala ya Ijuma ya Tehran pia amewapongeza wapigania uhuru na haki kote duniani hususan taifa la Iran kwa maadhimisho ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu na kusema, sababu muhimu zaidi ya kupatikana ushindi huo ni mshikamano wa taifa la Iran.
Hatibu wa muda wa Swala ya Ijuma ya Tehran amesema siasa za Marekani, mipango ya Israel na fedha za Saudi Arabia vinatumiwa kwa ajili ya kuzusha machafuko ya kisiasa, kijeshi na utovu wa maadili katika maeneo mbalimbali ya dunia. Ameongeza kuwa, maadui wanafanya njama kubwa za kutaka kuwa na ushawishi nchini Iran na kuzusha ghasia na machafuko katika nchi za Mashariki ya Kati kama Syria, Iraq, Lebanon, Yemen na Palestina lakini njama hizo zitagonga mwamba. Vilevile amelaani harakati za makundi ya kitakfiri na kigaidi yanayochafua jina la Uislamu na ameyataka mataifa ya Waislamu kuzima na kuzuia njama za makundi hayo na washirika wao za kutaka kuharibu fikra na ustaarabu wa Kiislamu.