Hamas yasisitiza kuharakisha kufikiwa ramani ya njia ya kitaifa ya Palestina
Mwakilishi wa Ofisi ya Kisiasa ya Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Palestina (Hamas) ametaka kuharakishwa kufikiwa ramani ya njia ya kitaifa ya Palestina.
Khalil Ismail al Haya amesema kuwa, Quds, msikiti wa al Aqsa na wananchi wa Palestina wanakabiliwa na vitisho na wapo hatarini kutokana na uungaji mkono wa Marekani kwa maghasibu wa Kizayuni. Kwa sababu hiyo amesema kuna udharura mkubwa wa kuharakisha mchakato wa kufikia ramani ya njia ya kitaifa inayokubaliwa na Wapalestina wote.
Al Haya ameongeza kuwa, harakati za Hamas na Fat-h zimefanya mashauriano ili kufikiwa mapatano kati ya makundi ya Palestina na kuongeza kuwa: Hamas na taasisi zilizo chini yake katika Ukanda wa Ghaza, Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan na nje ya Palestina zina uamuzi wa kimkakati kwa ajili ya kushiriki pamoja kisiasa na kufikia ramani ya njia ya kitaifa.
Viongozi wa Hamas na Jihad Islami za Palestina katika vikao vyao vya huko nyuma walisisitiza umuhimu wa umoja wa Palestina na kukamilisha mapatano ya kitaifa na kuafiki kivitendo maamuzi yaliyochukuliwa katika kikao cha Makatibu Wakuu wa makundi ya Palestina.