Amir wa Qatar asisitiza kuimarishwa uhusiano na Iran
Amir wa Qatar Sheikh Tamim bin Hamad al-Thani ametaka kuimarishwa uhusiano wa nchi yake na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
Amir wa Qatar aliyasema hayo Jumatatu mjini Doha alipokutana na kufanya mazungumzo Waziri wa Nishati wa Iran Reza Ardakanian na kuongeza kuwa kuna haja ya kuimarishwa ushirikiano wa kieneo baina ya nchi mbili. Katika kikao hicho, Ardakanian ambaye ni mwenyekiti mwenza wa Tume ya Pamoja ya Kiuchumi ya Iran na Qatar alimkabidhi Amir wa Qatar ujumbe maalumu kutoka kwa Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
Katika kikao hicho, wawili hao wamesisitiza kuhusu haja ya kuimarishwa uhusiano wa nchi mbali kwa mujibu wa maamuzi na mapatano yaliyofikiwa katika safari ya Amir wa Qatar nchini Iran mwaka jana.
Amir wa Qatar na Waziri wa Nishati wa Iran wamesema ushirikiano wa kwa nchi mbili unaweza kuwa na nafasi muhimu kwa ajili ya maendeleo endelevu na maisha bora pamoja na usalama wa watu wa Iran na Qatar. Aidha amesema ushirikiano wa kirafiki baina ya nchi hizi mbili jirani unaweza kuwa mfano wa kuigwa na nchi zingine.
Katika kikao hicho Amir wa Qatar amemuamuru Waziri wa Biashara na Viwanda wa Qatar Ali Al-Kulwari ambaye ni mwenyekiti menza wa Tume ya Pamoja ya Kiuchumi ya Iran na Qatar kutayarisha haraka nyaraka za uimarishwaji uhusiano wa kiuchumi baina ya nchi mbili