Maulamaa wa Muqawama wasisitiza kudumishwa mapambano dhidi ya maadui
Jumuiya ya Kimataifa ya Maulama wa Muqawama imesisitiza udharura wa kuendelezwa mapambano ya makundi ya muqawama dhidi ya senario za chuki za maadui dhidi ya ulimwengu wa Kiislamu.
Taarifa iliyotolewa na Jumuiya ya Kimataifa ya Maulama wa Muqawama mwishoni mwa mkutano wake hapo jana uliofanyika kwa njia ya mawasiliano ya intaneti imelaani hatua ya baadhi ya mataifa ya Kiarabu ya kuyapachika jina la ugaidi makundi ya muqawama na mauaji dhidi ya wanasayansi wa nyuklia.
Mkutano huo uliofanyika kwa anuani ya 'Intifadha ya Umma Katika Kukabiliana na Vikao vya Kuanzisha Uhusiano wa Kawaida na Utawala Haramu wa Israel' umesisitiza kwamba, Israel ni msababishaji wa vurugu, ukosefu wa amani, fitina ya aina yoyote na migogoro katika eneo la Asia Magharibi.
Sehemu nyingine ya taarifa ya mwisho ya mkutano wa Jumuiya ya Kimataifa ya Maulama wa Muqawama imepongeza hatua ya mataifa yanayopinga kuanzishwa uhusiano wa kawaida na utawala ghasibu wa Israel na wakati huo huo yamekuwa yakiliunga mkono taifa madhulumu la Palestina.
Akihutubia katika mkutano huo, Sheikh Naim Qassim, Naibu Katibu Mkuu wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Hizbullah ya Lebanon amesisitiza kuwa, mataifa ya Kiarabu ya Ukanda wa Ghuba ya Uajemi, hakuna wakati wowote ule ambapo yalikuwa pamoja na taifa la Palestina na hakuna wakati ambao yaliunga mkono muqawama na mapambano ya Palestina.