Hamas yasisitizia mapambano ya silaha dhidi ya Wazayuni
Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS imesisitiza kuwa, mapambano ya silaha dhidi ya utawala wa Kizayuni ambao ndiye adui mkubwa wa ubinadamu, Waislamu na Wapalestina, ndiyo njia pekee ya kupambana na kumshinda adui huyo mtenda jinai.
HAMAS ilisema hayo jana usiku kwa mnasaba wa kumbukumbu ya mashambulizi ya siku 22 yaliyofanywa na utawala wa Kizayuni dhidi ya wananchi wa Ukanda wa Ghaza na kusisitiza kuwa, muqawama hauna papara, lakini wakati wowote adui Mzayuni atakapofikiria kumwaga damu za Wapalestina, basi atakumbwa na majibu makali ambayo yatamuacha kinywa wazi.
Harakati ya HAMAS pia imesema, kuwakomboa mateka Wapalestina kutaendelea kuwa moja ya malengo makuu na matukufu ya harakati hiyo na kwamba maadamu Wazayuni wanaendelea kuwashikilia mateka Wapalestina, basi muqawama wa taifa hilo nao kamwe hautotulia hata kwa sekunde moja.
Taarifa ya harakati hiyo ya mapambano ya Kiislamu ya Palestina pia imesema, katika maadhimisho ya mwaka huu ya vita vya siku 22 vya mwaka 2008 vilivyoanzishwa na Israel dhidi ya Wapalestina wa Ghaza, muqawama wa Palestina uko imara zaidi na una silaha za kisasa zaidi huku kuwakomboa mateka wa Kipalestina likiwa ni moja ya malengo makuu ya HAMAS.
Tarehe 27 Disemba 2008, utawala wa Kizayuni wa Israel ulianzisha mashambulizi ya poande zote kwa lengo la kuisambaratisha kikamilifu Harakati ya Mapoambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS na vita hivyo viliendelea kwa muda wa siku 22. Vita hivyo ni maarufu kwa jina la mauaji ya umati ya Ghaza ambapo Wazayuni waliua kikatili zaidi ya Wapalestina 1,450 na kujeruhi zaidi ya 5,000 wengine katika kipindi hicho cha siku 22, lakini ilishindwa kuisambaratisha harakati hiyo ya Kiislamu.