Mamluki wa Saudia wahujumu harusi nchini Yemen, waua watu watano
(last modified Sat, 02 Jan 2021 13:01:09 GMT )
Jan 02, 2021 13:01 UTC
  • Mamluki wa Saudia wahujumu harusi nchini Yemen, waua  watu watano

Mamluki wanaoungwa mkono na Saudi Arabia wamevamia sherehe ya harusi katika mji wa bandarini wa Al Hudaydah nchini Yemen na kuua watu wasiopungua watano na kuwajeruhi wengine kadhaa wakiwemo wanawake saba.

Kaimu Gavana wa Al Hudaydah Muhammad Ayyash Qahim amesema hujuma hiyo imejiri Ijumaa usiku katika mtaa wa al Hawk. 

Ameongeza kuwa watu watano wamejeruhiwa katika hujuma hiyo wakati walipokuwa nje ya ukumbi wa harusi wakiwasubiri wake na watoto wao kwa ajili ya kurudi majumbani baada ya shughuli hiyo.

Qahim amelaani hujuma hiyo ya kinyama iliyotendwa na mamaluki wa Saudi Arabia na amesisitiza kuwa, kulenga eneo la raia ni jinai ya kivita inayokiuka sheria na kanuni zote za kimataifa. Imedokezwa kuwa mamluki hao wa Saudia wanafungamana na rais wa Yemen aliyejiuzulu Abdrabbuh Mansur Hadi.

Mapema mwezi uliopita wa Disemba,  Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kuratibu Masuala ya Kibinadamu (OCHA) ilitangaza kuwa vita vya Saudi Arabia dhidi ya Yemen vimepelekea zaidi ya watu 233,000 kupoteza maisha katika kipindi cha miaka sita iliyopita.

Wanawake na watoto ni waathirika wakuu wa vita vya Saudia dhidi ya Yemen

Ikumbukwe kuwa mnamo mwezi Machi 2015 Saudi Arabia, ikiungwa mkono na  Marekani, utawala haramu wa Israel, Umoja wa Falme za Kiarabu  na nchi zingine kadhaa iliivamia kijeshi Yemen na kuiwekea mzingiro wa kila upande.

Utawala dhalimu wa Saudia ulianzisha mashambulizi dhidi ya Yemen kwa lengo la kuiondoa madarakani Harakati ya Ansarullah na kumrejesha uongozini kibaraka wake, Abdrabbuh Mansour Hadi, rais wa zamani wa nchi hiyo aliyejiuzulu na kukimbilia Riyadh. Hata hivyo hadi sasa Saudia na washirika wake wameshindwa kufikia malengo yao kutokana na kusimama kidete wananchi wa Yemen.

 

Tags