Oxfam: Silaha za Uingereza zinazouzwa Saudia zinarefusha vita nchini Yemen
Shirika la misaada ya kibinadamu la Oxfam limetangaza kuwa, uuzaji wa silaha za Uingereza kwa utawala wa Saudi Arabia unarefusha vita vya muungano unaoongozwa na serikali ya Riyadh dhidi ya taifa la Yemen.
Oxfam imeituhumu serikali ya Uingereza kuwa inarefusha vita vya Saudi Arabia na washirika wake nchini Yemen kupitia njia ya kuiuzia nchi hiyo silaha na zana mbalimbali za kivita ambazo zinarahisisha mashambulizi zaidi ya anga dhidi ya Yemen.
Ripoti zimethibitisha kuwa silaha zinazotumiwa na Saudi Arabia na washirika wake dhidi ya taifa la Yemen ni kutoka nchi za Marekani, Uingereza, Ufaransa, Ujerumani na nchi nyingine kadhaa za Magharibi.
Mwezi Machi mwaka 2015 Saudi Arabia ikishirikiana na Imarati, Marekani, utawala haramu wa Israel na nchi nyingne kadhaa za Kiarabu na Kimagharibi zilianzisha mashambulizi makali dhidi ya taifa la Yemen na kuizingira nchi hiyo kutokea pande zote. Maelfu ya raia wa nchi hiyo wameuawa na mamilioni ya wengine wamelazimika kuwa wakimbizi ndani na nje ya nchi kutokana na masmabulizi hayo.
Hivi karibuni Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa anayehusika na masuala ya kibinadamu, Mark Lowcock alisema kuwa, Yemen inaelekea kwa kasi katika hali mbaya ya maafa makubwa ya njaa ambayo hayajawahi kushuhudiwa duniani katika miongo kadhaa iliyopita na kwamba karibu dola bilioni 4 zinahitajika ili kutekeleza oparesheni za kibinadamu na kuzuia njaa nchini humo.

Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO) Mfuko wa Kuhudumia Watoto wa Umoja wa Mataifa (UNICEF), Mpango wa Chakula Duniani (WFP) na Shirika la Afya Duniani (WHO) pia hivi karibuni yalitoa ripoti na kueleza kuwa, watoto wa Kiyemen laki nne walio na umri wa chini ya miaka mitano wako katika hatari ya kifo kutokana na njaa.