Jihadul-Islami ya Palestina: Hatutashiriki uchaguzi wa bunge
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i67318-jihadul_islami_ya_palestina_hatutashiriki_uchaguzi_wa_bunge
Mwanachama mwandamizi wa Harakati ya Jihadul-Islami ya Palestina amesisitiza kuwa, katika kuhakikisha inakwenda sambamba na msimamo wake wa kisiasa, harakati hiyo haitashiriki katika uchaguzi wa bunge la Palestina.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Feb 27, 2021 03:50 UTC
  • Jihadul-Islami ya Palestina: Hatutashiriki uchaguzi wa bunge

Mwanachama mwandamizi wa Harakati ya Jihadul-Islami ya Palestina amesisitiza kuwa, katika kuhakikisha inakwenda sambamba na msimamo wake wa kisiasa, harakati hiyo haitashiriki katika uchaguzi wa bunge la Palestina.

Sheikh Nafidh Azzam, ambaye ni mjumbe wa ofisi ya kisiasa ya harakati ya Jihadul-Islami ya Palestina amebainisha kuwa, kuondoka kwa Donald Trump ni funzo linalotoa ibra kwamba watu wote wajue kuwa mabavu na madaraka haviwezi katu kuishinda haki; na ni kwa sababu hiyo haipasi kwa wenye haki kusalimu amri bali waendelee kupigania haki zao.

Sheikh Azzam amesisitiza kuwa, Harakati ya Jihadul-Islami  haiwezi kubadilisha mipango na utambulisho wake, unaoitakidi kuwa jihadi na muqawama ndilo chaguo pekee la kistratejia kwa ajili ya harakati hiyo na wananchi wa Palestina.

Mwanachama huyo mwandamizi wa Jihadul-Islami amesema, utawala haramu wa Kizayuni wa Israel umetumia nyenzo zake zote kwa uungaji mkono wa pande za kikanda na kimataifa ili kulipigisha magoti na kulishinda taifa la Palestina, lakini haujaweza kulifuta jina la Palestina.

Msikiti mtukufu wa Al Aqsa

Sheikh Nafidh Azzam ameongeza kuwa, taifa la Palestina halitasalimu amri abadani; na irada ya taifa hilo, ambalo limechaguliwa na Mwenyezi Mungu kwa ajili ya kuulinda na kuuhifadhi msikiti wa Al Aqsa haitazimwa.

Mwezi uliopita wa Januari Rais Mahmoud Abbas wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina alitangaza ratiba ya kufanyika chaguzi za bunge, urais na baraza la taifa la Palestina; na kwa mujibu wa agizo alilotoa, uchaguzi wa bunge la Palestina utafanyika tarehe 22 Mei, uchaguzi wa rais wa Mamlaka ya Ndani utafanyika tarehe 31 Julai na ule wa baraza la taifa la Palestina utafanyika Agosti 31 mwaka huu.../